NIANZE kwa kukiri kwamba wanachama na
mashabiki wa Simba wana haki ya kumzomea kiongozi, kocha au mchezaji wanayekuwa
hawakubaliani na utendaji wake.
Mashabiki wanachotaka ni kuona kikosi chao
kinafanya vizuri. Kweli kuna matokeo ya mchezo wa soka ambayo hata hivyo
mashabiki wachache wa soka wamekuwa wakikubaliana nayo.
Wako ambao wamekuwa wakikubaliana nayo
lakini wako ambao wamekuwa wakishindwa kuvumilia kabisa kutokana na mateso
makubwa kwa klabu yao.
Mashabiki hawataji hata kuona mchezaji
anakosea, hii ni kawaida ndiyo maana ya kupeleka mambo kitaalamu na kishabiki.
Hivyo uache kila upande ufanya kazi kivyake.
Pamoja na kukubali hayo, kuna jambo moja
liliniumiza sana, nikataka kujua kwa undani kuhusiana na Kocha Msaidizi wa Simba,
Selemani Matola ambaye aliamua kuuambia uongozi angependa kupumzika.
Wakati Matola anasema vile, uongozi
ukamkubalia, lakini Kocha Mkuu, Goran Kopunovic akauomba uongozi wampe nafasi
ya kuzungumza na Matola, kweli akapewa nafasi hiyo, mwisho wakakubaliana na
kocha huyo msaidizi akakubali kubali.
Ajabu siku chache baadaye mashabiki wa Simba
wakamzomea Matola pale Uwanja wa Taifa jijini Dar. Wengine nikawasikia
wakihojiwa kwenye rekodi kuhusiana na kocha huyo.
Kilichonishangaza ni kusikia karibu kila aliyehojiwa
anasema kwamba Matola anawahujumu. Alipoulizwa anawahujumu vipi? Jibu lilikuwa
anampangia Kopunovic timu au anamshawishi wachezaji fulani wasicheze!
Majungu ya kijinga kabisa! Sikuamini
kinachoelezwa, nilijaribu kufuatilia kwa karibu, mwisho nikagundua tatizo hili
kuwa kuna kiongozi mmoja aliye ndani ya kamati ya utendaji haelewani na Matola.
Kiongozi huyo ambaye kwa uzoefu wangu wa
kuripoti habari za michezo, naanza kumuona akiwa na Simba au akiisaidia ndani
ya kipindi cha mwaka mmoja tu uliopita, si vibaya nikimuita mgeni.
Lakini anasifika kuwa na ukaribu na
wanachama wengi kwenye matawi. Hivyo ukimuudhi au kupingana naye, basi
anakupangia ‘mashambulizi’ ili uonekane mbaya mbele za watu. Mfano sasa
usishangae kuona Saleh Ally anazomewa sana na mashabiki wa Simba (he..he..he).
Najiuliza kiongozi huyo mgeni, au mashabiki
hao wa zamani na siku hizi, wanafikiri ni sawa kumzomea Matola kisa habari za
uzushi zisizokuwa na uhakika?
Kama ni kweli, Kopunovic angesema. Kama
kweli anampangia timu basi Simba imuondoea kocha mkuu maana hana msimamo.
Lakini kama angekuwa si sahihi, Mserbia huyo asingekubali Matola aendelee
kubaki naye.
Kama hayo yote si sawa, vipi Kopunovic
aliuomba uongozi wa Simba umpe nafasi ya kuzungumza na Matola licha ya yeye
kuomba aondoke?
Wanasimba wenye mapenzi na timu na klabu yao
hawawezi kumlipa Matola kwa njia hiyo. Aliichezea Simba iliyojaa shida,
wachezaji walikula kwa mama ntilie.
Aliendelea kubaki huku wengine wakikimbia
hadi ilipoimarika na kuwa timu bora iliyobeba makombe kibao mwisho ikaweka
rekodi ya kuing’oa Zamalek kwenye michuano mikubwa ya Afrika wakati huo ikiwa
bingwa na timu bora Afrika.
Yule kiongozi mgeni, wewe shabiki mna
chochote cha kujilinganisha naye? Je, mna uhakika kuhusiana na yanayozungumzwa
au mmebebeshwa tu kama ilivyo bendera na sasa mnafuata upepo?
Unajua kwamba takribani wachezaji 12 wa
Simba, ni vijana waliotoka katika kikosi cha vijana kilichosukwa na Matola hadi
kutwaa Kombe la Banc ABC kukiwa na timu kongwe kama Mtibwa Sugar na Azam FC?
Leo wachezaji hao makinda ndiyo tegemeo la
Simba tena wanafanya kazi nzuri hata kuliko wale wageni walionunuliwa
mamilioni.
Vipi mnakubali kuvaa ngozi ya chui kwa lengo
la kumfurahisha kiongozi mmoja tu na kusahau yote ya Matola ambaye ameifanyia
Simba lukuki mkifananisha na huyo kiongozi mgeni?
Mkubali mkatae, Matola atabaki kuwa shujaa
wa Simba milele na kiongozi huyo ataondoka. Hivyo kama uongozi umekubali
aondoke, mpeni heshima yake aende kwa amani kwa kuwa ameifanyia Simba makubwa
kuliko viongozi karibu wote wa Simba walio madarakani.
Tatizo mnaandika makala bila kufanya utafiti. Kubali ama ukatae, Matola bado ni tatizo Simba. Katika kufuatilia kwangu mpira, na pia niliwahi kuwaambia watu mwanzoni tu Sele alipoteuliwa kufundisha timu ya wakubwa. Nikasema aidha Simba wampe ukocha mkuu ama timu haiwezi kuwa consistent na matokeo mazuri. Sele alifanya vizuri na timu ya vijana akiwa kocha mkuu na si msaidizi, hilo unalisahau. Fanya utafiti wako kwa kuwaangalia Matora japo hana muda mrefu kweye ualimu wa soka, Marehemu Mziray na Julio, utangundua hawajawahi kufanya vizuri na timu yoyote wakiwa makocha wasaidizi. Wanaopiga kelele leo wanajua walimtumia vipi kipindi cha Rage na ndio maana wanahisi sasa amewageuka
ReplyDelete