Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI wa
Simba, Emmanuel Okwi amekuwa gumzo baada ya kufunga mabao mawili ‘matamu’
katika mechi mbili za Ligi Kuu Bara.
Okwi amefunga mabao
hayo katika mechi dhidi ya Yanga, Jumapili iliyopita. Akaonyesha hakubahatisha
tena kwa kufunga bao linalofanana na hilo Simba ilipoivaa Mtibwa Sugar,
Jumatano.
Aina ya mabao hayo
ambayo amefunga kwa umbali wa kuanzia mita 25 lile la Mtibwa Sugar na zaidi ya
mita 30 lile dhidi ya Yanga, umefanya yawe mabao gumzo zaidi katika kipindi
hiki.
Pamoja na kwamba
hakufanikiwa kufunga bao katika mechi dhidi ya Mgambo Shooting wakati Simba
ikilala kwa mabao 2-0 Mkwawani, Tanga, jana. Bado haizuii mabao aliyofunga
dhidi ya Yanga na Mtibwa kuendelea kuwa bora.
Katika mahojiano
maalum, Okwi amekiri kuwa amejifunza aina ya upigaji mipira kupitia kiungo
mchezeshaji hatari kutoka klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani, Marco Reus.
Huyu ndiye shujaa
na mchezaji kipenzi zaidi kwa Okwi. Raia huyo wa Ujerumani ni kati ya wachezaji
ambao wamekuwa wakiwaniwa na timu mbalimbali kama Real Madrid, Arsenal na
nyingine kubwa kadhaa.
Reus anajulikana
kwa uwezo mkubwa wa kuchezesha timu pia ufungaji wa mabao muhimu, jambo ambalo
Okwi amekuwa akitaka kulifanya kwa Simba.
Okwi tayari ana
mabao saba katika Ligi Kuu Bara. Lakini anataka kufunga zaidi kama nafasi
itapatikana.
SALEHJEMBE:
Kipi hasa kinakuvutia kwa Reus?
Okwi:
Ni mchezaji anayejiamini, hana hofu na anaijua kazi yake. Kwangu ndiye mchezaji
bora zaidi kuliko wote wanaocheza soka duniani.
SALEHJEMBE:
Kipi umechukua kutoka kwake?
Okwi:
Kwanza siwezi kuchukua kila kitu, kama mchezaji pia nina mambo yangu. Lakini
namna ya kumiliki mpira, pasi nzuri, kujiamini pia upigaji wa mashuti kama
ambavyo uliona tulivyocheza na Yanga na baadaye Mtibwa.
SALEHJEMBE:
Unajifunza kwa kuona tu, au kuna ziada?
Okwi:
Kwanza naangalia kazi zake, Dortmund ikiwa inacheza. Lakini kwenye You tube,
halafu nikiwa uwanjani nafanya kazi ya kupiga mipira. Nilikuwa nikikosea mingi,
sasa naanza kupatia zaidi.
SALEHJEMBE:
Unafikiri ulikosea mara nyingi hata katika mechi au mazoezini tu?
Okwi:
Hata katika mechi, naamini hata nilionekana kama sijui ninafanya nini. lakini
nilipania kufanikiwa na ilikuwa ni lazima nijaribu.
SALEHJEMBE:
Unafikiri utaendelea kufunga zaidi mabao ya aina hiyo?
Okwi:
Inawezekana au isiwe hivyo. Kikubwa ni kumuomba Mungu maana yeye ndiye kila
kitu. Lengo kubwa kwangu ni kufunga, nikishindwa basi nisaidie timu hata kutoa
pasi kwa wenzangu wafunge. Akifunga yoyote ni muhimu kwa timu.
SALEHJEMBE:
Unafikiri Simba ina nafasi ya
kutwaa ubingwa wa Ligi kuu Bara?
Okwi:
Nafasi ipo, kama tutaendelea kushinda, itakuwepo. Kikosi chetu ni kizuri na
matatizo madogo yanaanza kurekebishika. Imani yangu tutafanya vizuri, lakini
bado tunamuachia Mungu.
SALEHJEMBE:
Vipi kuhusu ufungaji bora?
Okwi:
Ninaweza kuwa mfungaji bora au hapana. Lakini zaidi naangalia Simba itapata
nini baada ya ligi. Ndiyo maana nilikuambia kufunga mimi sawa, nikitoa pasi
sawa. Lengo hasa ni kuisaidia timu na ikishinda mechi nyingi zaidi bila ya
kujali nani kafunga, ndiyo faida kubwa zaidi.
SALEHJEMBE:
Karibu sana Championi Okwi.
Okwi:
Nashukuru sana.









Na kujipoza baada ya machungu kunaruhusiwa .
ReplyDelete