NAAMINI utakuwa umesikia taarifa za mauaji ya Waafrika
ambayo yamekuwa yakiendelea nchini Afrika Kusini. Safari hii kwa mara nyingine
ni mauaji ya Waafrika wanaowaua Waafrika wenzao.
Kawaida, Afrika Kusini inajulikana kutokana na ubaguzi
wa rangi, weupe wamekuwa wakiwabagua weusi. Wakati mwingine wanawatesa kikatili
na hata kuwaua, jambo ambalo nchi jirani za Afrika Kusini, ikiwemo Tanzania,
zimepambana kweli kuliondoa.
Unakumbuka raia wa Afrika Kusini walioishi Tanzania
wakiwemo wale wa Morogoro? Lengo lilikuwa kuwapa nafasi ya kujipanga ili
waendelee kupambana hadi waikomboe Afrika Kusini, sasa wamekombolewa, wako huru
na wao wameanza kuonyesha walivyojifunza ubaguzi.
Wapuuzi hao wa Afrika Kusini wameanzisha mauaji ya raia
wa nchi nyingine za Kiafrika. Mauaji hayo maarufu kama Xenophobia, yamekuwa
yakiendelea katika sehemu mbalimbali za Afrika Kusini.
Waafrika wanasema Waafrika wenzao wanachukua kazi zao,
wanawanyima wao ajira. Mbaya zaidi si rahisi kusikia ameuawa Mzungu kutoka
Sweden, Uingereza au Uholanzi. Waafrika tu ndiyo wanaowabana Waafrika wenzao,
upuuzi wa karne zote.
Nchini Afrika Kusini, kuna michuano ya Ukanda wa Kusini
mwa Afrika (Cosafa). Inatarajiwa kuanza Mei 17, mwaka huu.
Tanzania ni kati ya nchi zilizothibitisha kushiriki
katika michuano hiyo ambayo itashirikisha timu za Botswana, Lesotho,
Madagascar, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Namibia, Shelisheli, Swaziland,
Zambia, Zimbabwe na wenyeji Afrika Kusini.
Kikosi chetu cha Taifa Stars kinakwenda katika
mashindano hayo kama mwalikwa kwa kuwa kipo katika ukanda tofauti chini ya
Cecafa. Tayari Rais wa TFF, Jamal Malinzi ameweka wazi hisia zake kuhusiana na
mauaji hayo kwa kutuma barua kwa Shirikisho la Soka la Afrika Kusini (Safa)
kuungana nalo kulaani mauaji.
Safa na TFF wamelaani mauaji hayo lakini hawajapinga
muendelezo wa Xenophobia. Upuuzi unaoendelezwa na hao wazembe wa Afrika Kusini
unapaswa upingwe kwa nguvu.
Ghana waliokuwa waalikwa, tayari wametishia kujitoa
katika michuano hiyo kama itaendelea. Naungana nao na wameonyesha kiasi gani
walivyo imara.
Siilaumu TFF, lakini nasisitiza imeonyesha msimamo
tofauti ukilinganisha na Tanzania tunavyojulikana. Iko haja ya kuweka msimamo thabiti,
hili si jambo dogo.
Hatuwezi kukosa lolote kwa kutoshiriki michuano hiyo ya
Cosafa ambayo hatujashiriki miaka zaidi ya 20. Haina faida kwetu kama
tunakubali kwenda kwenye ardhi iliyojaa damu ya Waafrika wenzetu wasio na
hatia.
Nimeishi Afrika Kusini katika Kitongoji cha Bryanston.
Najua tafrani za Jiji la Johannesburg, nimejifunza uharaka wa kuripoti uwanjani
kwa mafunzo ya vitendo katika Runinga ya SuperSport.
Nimesoma kozi zangu fupi za mafunzo ya kuripoti kwa
ufasaha katika Chuo Kikuu cha Unisa cha Pretoria, nimetembelea miji zaidi ya
minne nchini humo. Lengo ni kukuonyesha si mgeni Afrika Kusini.
Nawajua raia wa nchi hiyo, wengi ni wavivu, wasiopenda
kujituma, watu wenye kulalamika kila wakati, lakini ni watu wasiojua mapambano
ya maisha nje zaidi ya kwao.
Uzembe wao wa kutojituma ndiyo umewafanya wawe walivyo
na kusahau hata fadhila za Waafrika wenzao. Tuliona Wazungu waliowabagua weusi
walitengwa na jamii mbalimbali ikiwemo kuondolewa katika mashindano chini ya
Fifa na Caf.
Sasa vipi Tanzania inakubali kupeleka timu sehemu ambayo
Waafrika wanauawa? Vipi TFF inaingia na kusema inaungana na Safa kupinga badala
ya kueleza au kuweka msimamo wake thabiti kwamba inataka hivi na kama
haiwezekani basi?
Tunajua, kweli si Cosafa inayoua watu au Waafrika Kusini
wote wanaofanya hivyo lakini wengi wanaweza kutumikia adhabu ya wapuuzi
wachache kama hao wazembe wanaoua watu na TFF inapaswa kuwa imara na kuwa na
tafakuri jadidi hasa katika mambo yanayohusu uhai wa wanadamu. Wakiacha sawa,
kama wanaendelea, itoeni timu yetu.
0 COMMENTS:
Post a Comment