Kiungo mkabaji wa
Simba, Jonas Mkude, amepata pigo baada ya kufiwa na baba yake mzazi, Gerald
Jonas Mkude kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya figo, hivyo kiungo huyo
ameondoka Shinyanga jana Jumapili kurejea Dar es Salaam na kuukosa mchezo dhidi
ya Kagera Sugar unaotarajiwa kupigwa leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Kambarage,
Shinyanga.
Mzee Mkude alikuwa
akisumbuliwa na matatizo ya figo na alifikishwa katika Hospitali ya
Mwananyamala jijini Dar siku tatu kabla ya kufikwa na umauti huo jana Jumapili
akiwa katika hospitali hiyo ya Mkoa wa Kitatibu wa Kinondoni.
Mkude amesema kuwa,
baba yake alifariki saa 10 alfajiri ya jana Jumapili na mipango ya mazishi
itapangwa baada ya yeye kuwasili jijini Dar akitokea Shinyanga ambako timu yake
ipo kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar.
“Ni kweli mzee
amefariki leo (jana) saa kumi alfajiri katika Hospitali ya Mwananyamala pale.
Alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya figo na alipelekwa pale kama siku tatu hivi
nyuma kabla ya kufariki.
“Mungu akipenda
tunatarajia kuzika Jumatano (keshokutwa), lakini kupata uhakika kamili mpaka
nitakapofika Dar kutoka huku Shinyanga kwa sababu wananisubiri nifike ili
tupange utaratibu mzima wa mazishi,” alisema Mkude.
Wakati huohuo,
uongozi wa Simba kupitia kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans
Poppe, umesikitishwa na msiba huo na kusema kuwa wapo bega kwa bega na Mkude na
tayari wameshampa ruhusa ya kurejea Dar kuungana na familia yake.
“Uongozi wa Simba
tumepokea kwa masikitiko sana taarifa hizi, lakini Mungu ndiye mwamuzi, hakuna
wa kulaumiwa,” alisema Hans Poppe.
SALEHJEMBE, INATOA
POLE KWA MKUDE NA FAMILIA YAKE
MWENYEZI MUNGU
AILAZE MAHALI PEMA
0 COMMENTS:
Post a Comment