April 15, 2015



Na Saleh Ally
HAUWEZI kukataa kuwa kweli sisi wanadamu tumeumbwa na usahaulifu tena kupindukia.


Usibishe, hata kama umesahau basi jikumbushe namna ambavyo mashabiki wa Manchester United walivyokuwa wakilalama miezi minne tu iliyopita.

Mashabiki hao walitaka Kocha Louis van Gaal aondoke, waliona Wayne Rooney hafai kabisa huku wakipinga Manchester United kuendelea kubaki na Ashley Young na Antonio Valencia.

Wakati mashabiki wa Manchester United wakilalama, wenzao wa Arsenal ndiyo walionyesha wamechoka kabisa huku wakitaka baadhi ya watu kuondoka.


 Kocha Arsene Wenger ,alikuwa adui namba moja na kila mmoja alitaka aondoke. Kiungo Mesut Ozil alionekana hana msaada.

Mshambulia Olivier Giroud ndiye alionekana hafai kabisa, wakidai hajui kufunga na alionekana si shujaa wa timu hiyo.

Lakini leo Arsenal inashika nafasi ya pili, Manchester United iko katika nafasi ya tatu ya msimamo wa Ligi Kuu England.

Miezi michache baadaye baada ya wachezaji na makocha kuonekana hawana lolote, Man United wakionekana hawatashiriki hata Kombe la Europa, leo ndiyo wanaokonga nyoyo za mashabiki wao ambao wanawaunga mkono kwa kuwasifia kwelikweli.

Ukiachana na msimamo wa ligi, kuna msimamo wa kiwango maarufu kama “form table”. Yaani ndani ya mechi nane zilizopita, timu imeshinda mechi ngapi, imepoteza ngapi na sare ngapi. Arsenal na Man United ndiyo zinaongoza.

Katika mechi nane, Arsenal haijapoteza mechi hata moja huku ikiwa imebeba pointi zote 24. Man United imepoteza mechi moja tu katika nane, imebeba pointi 21.

Chelsea iko katika nafasi ya tatu katika msimamo huo baada ya kushinda mechi sita na kutoka sare mbili. Imechukua pointi 20.

Hivyo katika “form table”, Arsenal inaonyesha ndiyo timu bora zaidi katika kipindi hiki ikifuatiwa na Man United.

Chelsea ambayo iko kileleni mwa ligi hiyo, inaendelea kupambana kwa kuwa angalau inaweza kupambana na timu hizo mbili huku Manchester City ikionekana kupotea katika msimamo ikiwa nafasi ya saba kwenye msimamo huo wa kiwango kwa kuwa katika mechi nane, imeshinda nne na kupoteza nne, hivyo imepata pointi 12 na kupoteza 12.

Katika mechi hizo nane, Man United imefunga mabao 19, Arsenal mabao 18 na Chelsea imetikisa nyavu mara 12 tu.

Safu za ulinzi; Arsenal imefungwa mabao matano tu, Chelsea 6 na Man United 7. Hii inaonyesha kwamba timu hizo ziko katika kiwango cha juu kabisa.

Mwendo wanaokwenda nao sasa unaonyesha kuwa ni watu wanaojituma lakini kwa mashabiki wanatakiwa kujifunza jambo kwamba wakati mwingine uvumilivu unahitajika.

Wale waliolalamika kuhusiana na Marouane Fellaini, nani angekuwa msaada wa kiungo cha Mashetani hao kama sasa kama angeondoka?

Mashabiki wajue, katika timu kuna mambo hujitokeza lakini lazima mashabiki wajue kuwa wachezaji nao ni binadamu na wanaposhindwa si makusudi.

Kuamini kirahisi tu, eti Wenger hafai au Giroud hajui kufunga nalo si sahihi. Ndiyo maana leo nimeamua kuwakumbusha baada ya kuona mmesahau kabisa, tena siku chache zilizopita namna mlivyokuwa mkilalamika kwa kuwaona hawa jamaa hawafai kabisa.



                                GP       W          D       L       GF     GA      GD      Pts
1. Arsenal                8           8           0       0       18       5        +13      24
2. Man Utd               8          7            0       1       19       7        +12     21
3. Chelsea               8           6            2       0       12       6       +6       20
4. Liverpool              8           6            0       2       14       9       +5       18
5. C. Palace             8           5            1       2       16       9       +7       16
6. Swansea              8           4            1       3       10       9       +1       13
7. Man City               8           4            0       4       18       10    +8       12
8. Southampton        8           3            2       3       6          5      +1      11
9. Everton                 8           3            2       3       9          9       0        11
10. Tottenham         8            3            2       3       13       15      -2       11


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic