April 15, 2015


Yanga sasa wameamua kushinda mechi yao ya kwanza dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia. Unaweza kusema “iwe, isiwe”.

Uongozi wa Yanga umepanga mechi hiyo ipigwe mchana jua kali. Itaanza saa 9 Alasiri, hali ambayo inaonyesha lengo ni kuwapa Waarabu hao wa Afrika Kaskazini wakati mgumu kama jua litakuwa kali.

Yanga inashuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, Jumamosi kuwavaa Etoile katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho.



Kwa kawaida, Mji wa Sousse nchini Tunisia wanaotokea Etoile du Sahel, sasa una hali ya baridi. Hivyo Yanga wanataka wakutane na joto la Dar, ingawa ni kuomba siku hiyo iwe hali ya joto.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro, amesema wameamua kuwa mchezo huo uchezwe muda huo ili kuweza ‘kuwawini’ wapinzani wao.

Muro alizidi kufafanua kuwa, muda huo utakuwa muafaka kwao na wameona ni sahihi na wamekubaliana, huku kikosi kikiendelea na mazoezi katika Uwanja wa Taifa ili kujiimarisha zaidi kuelekea mchezo huo.

“Uongozi tumeamua kuwa mchezo wetu dhidi ya Etoile du Sahel utachezwa majira ya saa tisa alasiri siku ya Jumamosi, tumejipanga kama timu na lengo ni kufanya vyema na kuwa na matokeo mazuri hapa nyumbani kwanza kabla ya ugenini.

“Wapinzani wetu kwa sasa kwao kuna baridi sana, hivyo wanavyokuja kwetu kunakuwa na mabadiliko kwa kiasi kikubwa kwa sababu ni kipindi cha joto na sisi tukienda kule ina maana lazima tutakutana na hali ya baridi, hivyo ni bora kuweka mipango sawa mapema,” alisema Jerry.

Kikosi hicho cha Waarabu hao, kinatarajiwa kutua nchini leo Jumatano kwa ajili ya mchezo huo na inaonekana tayari kinajua kuwa kitachezeshwa katika jua kali.

Mmoja wa maofisa wa Etoile, Mohammed Mustafa, ameliambia gazeti hili kuwa, wana taarifa kwamba mechi yao itachezwa mchana.

“Kweli mechi itachezwa saa tisa alasiri. Tunajua na tumeshapewa taarifa. Sisi pia tunajiandaa,” alisema Mustafa alipozungumza kutoka Sousse, Tunisia huku akisisitiza tayari kikosi chao kimeng’oa nanga kuanza safari ya Dar es Salaam.

Ingawa alikataa kuelezea watajiandaa vipi, imeelezwa siku moja kabla ya kuondoka Tunisia, timu hiyo ilifanya mazoezi saa saba mchana wakati wa jua.  Hata hivyo, bado halikuwa jua kali sana lakini watakapowasili Dar es Salaam, watafanya mazoezi saa nane hadi tisa mchana.

Yanga imefanikiwa kufika hatua hiyo baada ya kuwang’oa BDF IX ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2, kisha wakakutana na FC Platinum ambapo waliichapa jumla ya mabao 5-2 na sasa kibarua ni dhidi ya Etoile, Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic