MIEZI michache ijayo, mimi na wewe
msomaji tutakuwa tumesimama kwenye foleni kwa ajili ya kupiga kura ili tuchague
viongozi wetu watakaotuongoza kwa miaka mingine mitano ijayo.
Najua, tunapishana au kufanana
kuhusiana na hisia au kuamini kwamba ni kiongozi yupi sahihi na anapaswa kutuongoza.
Acha tusubiri hiyo foleni kwa kuwa kila kitu ni majaaliwa.
Lakini wakati huu wa uchaguzi mkuu,
kuna kila aina ya mbinu zinazotumiwa na wanasiasa kwa ajili ya kuhakikisha
wanatimiza malengo yao.
Wanachoangalia ni kipi ambacho kinaweza
kuwapatia nafuu ya kuwapata watu ambao watawapigia kura za ushindi washinde
ubunge au vyeo vingine vitakavyokuwa vinagombewa.
Wanaopiga kura ni watu, ili kuwapata
lazima uwavute na wanachokipenda hata kama watakuwa hawakupendi wewe. Michezo
ni kati ya nguvu kubwa katika mioyo ya Watanzania.
Wanasiasa wanalijua hilo na wapo wengi
sana wamekuwa wakiitumia michezo kama sehemu ya kurahisisha mambo yao hasa
inapofikia wanataka kushinda.
Wapo ambao wamekuwa wakionyesha mapenzi
au kutaka kuisaidia michezo tokea awali. Yaani hata kabla ya uchaguzi na baada
ya uchaguzi. Hapa kuna makundi mawili ya wanasiasa.
Wale ambao huisaidia michezo kwa lengo
la kupata kura washinde, halafu hata baada ya hapo wanaendelea kutoa msaada.
Kundi la pili ni lile ambalo linasaidia kutaka kupata ushindi, likifanikiwa,
linaachana kabisa na michezo kwa kuwa limepata linachotaka.
Kundi la pili ndiyo kubwa zaidi, hata
sasa inawezekana litakuwa linajipanga ili liwatumie wanamichezo na michezo kwa
ajili ya kupata kura na kuendelea mbele huku likiwa halina habari na michezo
kabisa.
Michezo ina nguvu, michezo ni ajira,
michezo ni afya na msaada mkubwa kwa taifa letu. Wanasiasa walaghai wamekuwa
wakiitumia na kuiacha kama mwanaume anapoamua kutupa soksi zake zilizochakaa
kwa kuwa na matundu kibao.
Jiulize anayetaka kukamua maziwa ya ng’ombe
bila ya kufikiria kumpa chakula kizuri ili kuhakikisha anaweza kuhimili
vishindo vya kukamuliwa, anataka nini?
Wanasiasa wengi ni watu wanaojali wanachotaka,
wanaojali nafsi zao, wanaoangalia faida ya maisha yao na si vitu vingine
vinavyowasaidia au vilivyowawezesha kupata ushindi. Wanasiasa wengi ni
wabinafsi.
Kuna mifano mingi ambayo tumekuwa
tukiiona, mfano timu au bondia fulani akiwa anajiandaa katika michuano ya
kimataifa au mechi kali dhidi ya bondia kutoka Marekani au China, kamwe hauwezi
kuona akiwa mazoezini na mwanasiasa yeyote.
Wakati huo hauwezi kuwa bora kwa
wanasiasa kuona watafaidika. Wanajua wakiingia watagharimika, au wakiingia bondia
akapoteza itaonekana wao si watu imara wanaoweza kusababisha ushindi.
Kama atashinda au timu itashinda, basi
unakuwa ni wakati bora kabisa kwa wanasiasa kujisogeza, kulazimisha kuonekana
kwenye picha wakiwa naye na ikiwezekana hata kutoa zawadi kadhaa kwa madai
wanapongeza.
Wanasiasa siku zote wanapenda kushiriki
katika vilivyoiva, kamwe si katika kulima au upishi. Ndiyo wamekuwa wakiifanya
hivyo michezo ambayo ‘inaishi’ ikiwa na viwanja duni, vifaa vya hovyo, vijana
wasio na viwanja vya kuchezea! Lakini wanataka wawatumie wakati wanapoona
wanahitaji kushinda.
Wanasiasa wanaamini wao wana akili
nyingi kuliko viumbe wote duniani. Wanaamini hivyo kwa kuwa tu wamekuwa
wakitumia uongo uleule miaka nenda rudi na bado unawasaidia kutimiza ndoto ya
wanachokitaka.
Rasmi natangaza, kamwe sitakubali kuona
wanasiasa waongo, wasio na mawazo ya kuiendeleza michezo halafu waitumie kwa
ajili ya faida za matumbo yao wakati hawakufanya lolote kuisaidia kabla.
Najua nitawaudhi wanasiasa wengi,
lakini nitasema ukweli. Ninawaamsha wanamichezo kwamba hawana sababu ya
kutumika kwa misaada isiyo na tija ili wawasaidie hata wanasiasa wasio na uwezo
kupita ndani yao na kupata nafasi ya kuingoza nchi yetu.
Hakuna ubishi unajua, wanasiasa wangapi
walishiriki kusaidia michezo na wakati gani. Wale ambao hawakuijali, hakuna
haja ya kushirikiana nao, acheni waende njia zao ambazo waliamini ni sahihi.
Watatumaliza, amkeni, msikubali.







0 COMMENTS:
Post a Comment