Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), kupitia kwa kamati yake ya waamuzi, limesema lililazimika
kuwapangua baadhi ya waamuzi wa ligi kuu kutokana na kukwepa hujuma katika
kipindi hiki cha mwisho wa ligi.
Ligi kwa sasa
inaelekea ukingoni huku Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 46, Azam inashika
nafasi ya pili ikiwa na pointi 38.
Timu hizo zipo kwenye vita kali ya kuwania
ubingwa lakini pia Simba hawapo mbali wakiwa na pointi 35, huku wakiiombea Azam
ipate matokeo mabaya ili waweze kuipiku na kumaliza kwenye nafasi ya pili na
kupata nafasi ya kucheza michuano ya kimataifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama, alisema
walifikia hatua hiyo ya kuwabadilisha waamuzi hao baada ya kuona kuna uwezekano
mkubwa wa kuruhusu mianya ya hujuma ifanyike kirahisi kutokana na viporo
vilivyokuwepo kwa Azam na Yanga.
Alisema kuwa
waligundua kuna baadhi ya waamuzi wangechezesha timu moja kwenye mechi mbili
zinazofuatana, kitu ambacho ni kinyume na sheria za uamuzi kwani ingekuwa
rahisi mwamuzi huyo kutumika katika kupanga matokeo.
Alifafanua kuwa
sheria za uamuzi zinaelekeza kwamba mwamuzi akichezesha mechi haruhusiwi
kuchezesha nyingine inayoihusu timu moja kati ya hizo mbili mpaka ipite miezi
miwili kutokana na kukwepa hujuma.
“Kisheria mwamuzi
kaichezesha mfano Yanga leo, basi asiichezeshe tena mechi yoyote
itakayoihusisha timu hiyo mpaka miezi miwili ipite, hii ni kuepuka hujuma
zozote zile kutoka kwa mwamuzi huyo, hivyo vile viporo vya Yanga na Azam
vingewafanya waamuzi kutolikwepa hilo ndiyo maana tumewabadilisha,” alisema Chama.
0 COMMENTS:
Post a Comment