NILIKUWA uwanjani jijini Alexandria nchini
Misri wakati Yanga walikuwa wakipambana vilivyo na Al Ahly katika mechi ya Ligi
ya Mabingwa Afrika.
Yanga waling’olewa kwa mikwaju ya penalti
baada ya kufungwa bao 1-0. Mechi ikaongezewa muda na baadaye penalti ambazo
ziliwatoa Yanga.
Yanga ndiyo walikuwa na nafasi ya kushinda
mara mbili, wakianzia kwa Mbuyu Twite, akakosa na baadaye ikawa zamu ya Said
Bahanuzi, naye akakosa, mwisho Waarabu hawakufanya makosa.
Nilikuwa nimeketi pembeni ya runinga
nikishuhudia mechi kati ya Yanga dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
Yanga ilikuwa ugenini kupambana katika
Uwanja wa Olimpiki mjini Sousse, Tunisia. Ikafungwa bao 1-0 na kung’olewa
katika michuano hiyo ikiwa ni baada ya sare ya bao 1-1 jijini Dar es Salaam.
Sitaki kukubaliana na hadithi, eti Yanga
iliisumbua Al Ahly kwa kuwa ilikuwa imechoka. Tumeona ilikwenda Kombe la
Shirikisho, ikaingia hadi fainali.
Bado hauwezi ukasema Yanga imeibahatisha
Etoile na imeikosea kidogo tu kwani ilikuwa ina uwezo wa kuing’oa katika
michuano yao pamoja na kujiandaa kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha wanashinda
mechi hiyo muhimu ya kurudiana dhidi ya Yanga.
Inawezekana kwa kipindi hiki, Yanga inaweza
kuwa dira ya mwamko wa soka la Afrika Mashariki kutokana na mwenendo wake
ulivyo.
Mara mbili, Yanga inatolewa na timu za
Afrika Kaskazini ambazo zinajulikana kuwa zina uwezo mkubwa kutokana na
kuwekeza kwake katika michezo katika kiwango cha juu.
Unajua Waarabu walivyowekeza katika soka,
tena kitambo. Tunajua hali hiyo namna ambavyo imekuwa ikisaidia ubora wa timu
zao kuwa juu.
Kupambana kwao ni kwa hali ya juu, wana
mbinu za kila aina. Pamoja na kwamba tumekuwa tukilaumu kwamba wana fitina,
lakini uwezo wao uko juu.
Wana timu nzuri za watoto, vijana. Wana
viwanja bora vya kuchezea. Unaweza kusema mambo yao ni kama Ulaya kwa asilimia
kubwa ndiyo maana timu zetu zikisafiri kwenda Afrika Kaskazini, mara nyingi ni
kipigo hadi cha mabao matano au zaidi.
Lakini kama ulibahatika kuangalia mechi hizi
mbili za Yanga, ile ya Misri msimu uliopita na hii ya juzi dhidi ya Etoile
utagundua kuna tofauti kubwa.
Yanga ilicheza soka safi na kuwapa Waarabu
wakati mgumu. Hakuna aliyehofia kama ilivyokuwa awali na huenda licha ya kuwa
nyumbani, Etoile walikuwa na wakati mgumu sana.
Yanga ilishambulia mfululizo na kuwapa
wakati mgumu. Wakati mwingine walilazimika kucheza kwa umakini mkubwa huku
wakijilinda kuhofia wasipoteze dhidi ya Yanga.
Kweli Yanga imetolewa, lakini kiwango dhidi
ya Al Ahly na Etoile ndani ya misimu miwili jambo la kulitupia macho na
kulifanyia kazi. Kama kiwango hicho kitadumishwa, basi msimu ujao inaweza
kufika mbali.
Kama kikosi kitafanyiwa marekebisho husika,
uongozi wa Yanga utaendelea kuwa imara. Ule uisoyumba, basi lahisi mambo kwenda
vizuri hapo baadaye.
Kuwaangusha Waarabu haiwezi kuwa hadithi ya
siku moja. Lazima kuwe na mabadiliko taratibu. Maana yake Yanga imeingia katika
anga ambazo inaweza kuhimili mikiki ya Waraabu. Imekuwa ikikosea kidogo tu ili
kuwalipua kama itakutana nao.
Wao wamejipanga siku nyingi ukilinganisha na
nchi za ukanda wa Afrika Mashariki. Mabadiliko kama hayo, yatasaidia timu zetu
kuzidi kuimarika.
Kikubwa Yanga wahakikishe hakuna mvurugiko
katika kikosi chao. Pia kazi ya kusaka vijana, kuwa na utaratibu mzuri nayo iingie
kwenye programu.
Kuna kila sababu ya kuamini kuna mabadiliko
yanakuja kama timu kama Yanga leo inakwenda kucheza Uarabuni haina tena hofu
kufungwa bao tano au saba. Hiki ndiyo kipindi muhimu cha kuendeleza mapinduzi
ya soka hapa nyumbani. Mwendo wa Yanga ni njia sahihi.
Kweli kabisa mwandishi,tukiacha ushabiki hawa watani zetu wana soka la hali ya juu pengine tunaweza kusema ni tishio kwa club za africa mashariki,sioni kama kuna tofauti sana na TP mazembe,nina uhakika mwakani watafanya vizuri sana kama hawatatibuana.Hongera sana YANGA.
ReplyDelete