Na Saleh Ally
USHINDI wa pointi wa bondia Floyd Mayweather dhidi ya Manny Pacquiao
umezua gumzo kubwa huku wengi wakiamini Pacquiao, alishinda ila ameonewa!
Mabondia hao walioingia kwenye gumzo la miaka mitano mfululizo kuwa
watakutana lini au itakuwaje wakikutana, wamekata mzizi wa fitina baada ya
kukutana jana na Mayweather raia wa Marekani kushinda kwa pointi 118-110,
116-112, 116-112.
Kitaalamu katika mchezo wa ngumi inajulikana kama ‘unanimous
decision’. Yaani majaji wote watatu walimpa ushindi bondia mmoja na alikuwa
Mayweather.
Ushindi wa Mmarekani huyo kutoka kwa majaji wote umezua gumzo kubwa
miongoni mwa mashabiki na huenda wapenda ngumi wa Tanzania ndiyo wanaonekana
kutoamini kama kweli Mayweather ameshinda.
Wanasema amebebwa na mifano mingi kwamba Mayweather alitumia muda mwingi
kurudi nyuma. Hivyo waliamini hakuwa mshindi ila majaji “wamembeba.”
Pambano la raundi 12 la wakali hao lililopigwa katika Jiji la Las
Vegas, Marekani katika mji mdogo wa Sin City, lilithibitisha kuwa kweli
mabondia hao ni bora kabisa.
Mayweather alipanda ulingoni akiwa amepania kuendeleza neno “zero”.
Alikuwa amecheza mechi 47 bila ya kupoteza hata moja.
Ushabiki:
Umakini mkubwa wa Mayweather huenda ulifanya wengi waamini
amezidiwa. Walioangalia kwa jicho la juujuu pia waliamini ngumi nyingi zisizo
na pointi za Pacquiao ‘zilimkamata’ Mayweather ambaye ushindi wake una tofauti
kubwa ya pointi.
Pacquiao alionekana kuwa na papara muda mwingi na hata ngumi
alizopiga, nyingi ziliishia kifuani mwa Mayweather, mabegani au hata tumboni.
Lakini ngumi za Mayweather, nyingi zilionekana ni zenye malengo na
zilimsaidia kupata pointi nyingi.
Huenda inakuwa vigumu kuwaelewesha mashabiki wengi wa ngumi namna
hesabu zinavyopatikana lakini “score” katika mchezo wa ngumi inapatikana usoni
na atakayepata nafasi anaweza kurudia pambano hilo na kuona Mmarekani huyo
alivyochota pointi nyingi.
Katika kila sehemu walioangalia mashabiki wengi ikiwa ni pamoja na
kwenye Ukumbi wa MGM Grand, Las Vegas, walikuwa wakimshangilia sana Pacquiao,
kwa kila ngumi aliyorusha bila ya kujali imetua wapi.
Ziro:
Mayweather alikuwa mjanja na mtulivu, alijilinda zaidi na kupiga
ngumi zenye ‘macho’ ambazo zilimpatia hesabu nzuri zaidi.
Alitaka ziro iendelee kwenye rekodi yake na kweli amefanikiwa
kupigana na kushinda 48-0. Hii ilimfanya awe makini zaidi kuepuka mbinu za
Pacquiao ambaye alimuelezea kuwa mmoja wa mabondia bora duniani, ndiyo maana
alikuwa makini zaidi.
Ufundi:
Mayweather alijua anachotaka, ndiyo maana alikuwa bora zaidi
kiufundi. Wapo wanaoamini majaji watatu hawakuwa makini.
Wawili walimpa Pacquiao ushindi katika raundi 4, 6 na 10. Mmoja
akampa ushindi raundi mbili za 4 na 6. Zilizobaki alishinda Mayweather.
Kama majaji hao walikosea, basi takwimu za pambano hilo zinaonyesha
kumbana Pacquiao huku zikimpa sifa ya bondia bora ya siku ya pambano,
Mayweather.
Mayweather ndiye aliyerusha ngumi nyingi zaidi ambazo ni 435
ukilinganisha na 429 za Pacquiao. Wastani wa ubora hapo ni 34% kwa Mayweather
baada ya ngumi zake 148 kumfikia mpinzani wake huku Pacquiao akifikisha ngumi
81 tu ambazo ni 19%.
Jab ni zile ngumi za kudokoa zinazotua, hasa usoni. Mayweather
amepiga 267 na 67 zikafika na Pacquiao alirusha 197 na 18 zikafika. Hii huenda
ilitokana na mambo mawili, kwanza urefu wa Mayweather pia Mmarekani huyo
alikuwa mjanja na kukaa mbali na mpinzani wake kwa muda wote wa pambano.
Ule umakini wa ulinzi ndiyo ulifanya kazi kubwa hapa huku ukimpa
nafasi Mayweather kushambulia zaidi.
Katika ngumi, kuna ngumi kali na laini. Mayweather alirusha ngumi za
nguvu 168 na 81 zikamfikia mpinzani wake. Pacquiao akarusha 236 ambazo ni
nyingi zaidi kwa kuwa alikuwa akishambulia muda mwingi zaidi lakini akafikisha
63.
Wapo wanaoweza kuelewa kwamba pambano hilo kiufundi alikuwa juu
sana. Lakini wapo ambao hawaelewi kutokana na kutojua hesabu za mchezo wenyewe,
lakini wapo wanaoelewa lakini ni ile hamu tu ya kuona angalau Pacquiao naye
anashinda.
Kawaida binadamu wana kawaida ya kutofurahia mtu mmoja kutamba muda
mrefu hata kama ni juhudi zake binafsi. Mfano utakuwa umeona kwa Juma Kaseja au
msanii Diamond ambao wakati mwingine huchukiwa tu.
Upole, tabasamu la Pacquiao huenda vimekuwa moja ya vitu
vinavyowavutia wengi kuona anamshinda Mayweather mwenye mbwembwe na majivuno.
Zote zinaweza kuwa hisia, lakini hali halisi zinaonyesha kwa ngumi
za kishabiki, Pacquiao alikuwa bora zaidi katika pambano hilo lakini kwa ngumi
za ufundi, nafasi ilikuwa kwa Mayweather, ndiyo maana ushindi wake umekuwa
mkubwa.
TAKWIMU:
Mayweather
Pacquiao
435
Jumla ya ngumi
429
148
Ngumi zilizotua
81
34%
ASILIMIA
19%
Mayweather
Pacquiao
267
Jumla ya jab
193
67
Jab zilizotua
18
25%
ASILIMIA
9%
Mayweather
Pacquiao
168
Ngumi za nguvu
236
81
Ngumi zilizotua
63
48%
ASILIMIA
27%
0 COMMENTS:
Post a Comment