Bondia Mtanzania, Francis Cheka, anatarajia kuwasili jijini Dar
leo Jumatano akitokea mkoani Morogoro ambapo alikuwa akifanya mazoezi ya
kujiandaa na pambano lake dhidi ya Mthailand, Kitschai Singwacha
litakalofanyika Jumamosi ya wiki hii kwenye Ukumbi wa Sabasaba PTA, Dar.
Huku Cheka akitarajiwa kuwasili leo, mpinzani wake anatarajiwa
kuwasili kesho Alhamisi mchana ambapo mbali na pambano hilo la raundi kumi,
mabondia wengine watakaopanda ulingoni siku hiyo ni Kasim Ouma kutoka Marekani
ambaye atapigana na Mtanzania, Shaban Kaoneka, huku Mtanzania mwingine, Cosmas
Cheka akidundana na Mkenya, Fred Nyakes.
“Ninatarajia kuingia jijini Dar Jumatano (leo) tayari kwa pambano
hilo ambalo nina imani nitaibuka na ushindi kutokana na maandalizi
niliyoyafanya,” alisema Cheka.
Pambano hili la kihistoria, limedhaminiwa na Kampuni ya Global
Publishers, Pepsi na Fore Plan Clinic.
0 COMMENTS:
Post a Comment