Siku chache baada ya aliyekuwa winga wa Mbeya City, Deus Kaseke kusajiliwa
na Yanga, kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, amefunguka
kuwa, anafurahi kumpata mchezaji huyo kwa kuwa aliacha mapendekezo asajiliwe.
Winga huyo amepewa mkataba wa miaka miwili mara tu baada ya
kumaliza mkataba na timu ya awali ambayo ameitumikia kwenye ligi kuu kwa misimu
miwili tangu ilipopanda daraja 2013/14.
Akizungumza kutoka nchini
Ghana, kocha huyo alisema kuwa kwa sasa yupo mapumzikoni na familia yake lakini
anafurahi kwa kuwa alichopendekeza kimefanyiwa kazi.
Kocha huyo aliyeipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara,
alisema kuwa atarejea mapema nchini na hapo ndipo atapata nafasi ya kuzungumzia
zaidi masuala ya usajili.
“Siwezi kuzungumza sana, kwa sasa niko mapumzikoni lakini ukweli
ni kwamba alikuwa ni mmoja wa wachezaji niliokuwa nawahitaji kwenye kikosi
changu na nilimpendekeza katika ripoti yangu, mengi zaidi tutazungumza
nitakaporejea nchini mwezi Juni,” alisema Pluijm.
Winga huyo mwenye kasi na aliyefanikiwa kuichezea Mbeya City kwa
mafanikio makubwa licha ya msimu uliomalizika timu yake kuonekana kusuasua,
aliziingiza vitani klabu za Simba na Yanga zote zikiwania saini yake.
0 COMMENTS:
Post a Comment