Wadhamini wa Ligi Kuu Bara, Kampuni
ya Simu za Mikononi ya Vodacom imemaliza mkataba wake wa miaka mitano ya
kuidhamini ligi hiyo, hiyo ni hadi mwishoni mwa msimu huu.
Imeelezwa, tayari makampuni mbalimbali yamegongana katika ofisi za Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF), yakitaka kudhamini katika kipindi kingine kijacho.
Ligi Kuu Bara inatarajiwa kufikia tamati Mei
9, mwaka huu, wakati huo Vodacom itakuwa imemaliza mkataba wake wa miaka mitano.
Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine, amesema hadi
sasa wamepokea maombi lukuki kutoka kwa makampuni mbalimbali kutaka kuidhamini
ligi kuu baada ya kuona wadhamini wa sasa mkataba wao umeisha.
“Ni kweli Voda wamemaliza mkataba wao wa
kuidhamini ligi kuu na tayari hadi sasa kuna makampuni mengi ambayo
yamejitokeza kutaka kudhamini katika kipindi kijacho, lakini hatuwezi kuyataja
hadi hapo mambo yakapokaa sawa.
“Kwa jinsi sheria ya kimkataba ilivyo, lazima
kwanza tuanze kuzungumza na wadhamini wa kwanza ambao ni Vodacom, kisha ndiyo
tuwape nafasi wengine.
“Makampuni mengi yanahitaji kutangaza bidhaa kupitia
ligi kwani hakuna kampuni inayokataa kujitangaza, ila kwa sasa siwezi kutaja ni
makampuni mangapi yamejitokeza,” alisema Mwesigwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment