Na Saleh Ally
SAKATA la suala la mkataba wa kiungo mshambuliaji wa Simba,
Ramadhani Singano ‘Messi’, bado halijapata mwafaka kwamba tatizo ni nini hasa.
Ukisikiliza maneno ya wadau wa soka, anzia Simba, upande wa Messi
utasikia mengi sana ambayo yanaweza kukushangaza.
Wapo wanaosema Messi amegushi, wapo wanaoamini Simba wamemuonea na
ndiyo wamefanya mchezo mchafu. Lakini wapo wanaosifia kila upande, wakiamini
ndiyo upo sahihi.
Lakini sakata hilo linavyokwenda, inaonekana kuna kitu ambacho
huenda si kidogo kwa kuwa hata linavyopelekwa ni kutoka dogo kwenda kuwa kubwa.
Mfano ni baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuamua
kuingilia na kukutanisha pande zote mbili kulimaliza.
Mwisho wa kikao, kila mmoja akasema lake, TFF lao, Simba lao na
Messi la kwake. Mkanganyiko ukawa juu zaidi hata kuliko ilivyokuwa awali.
Wapo viongozi wa Simba wanalalamika, kwamba TFF inaonyesha ina nia
mbaya nao. Kwa kuwa mkataba wa Simba waliosaini na Messi, unalingana kabisa na
ulio TFF ambao ndiyo mkataba mama.
Lakini mkataba alionao Messi ambao ni kopi, haufanani hata kidogo
na ule ulio TFF na walionao Simba. Lakini wanashangazwa kuona TFF inashindwa
kutoa tamko hadi kusababisha mkanganyiko na watu wengi kuanza kupata hisia
Simba imefanya usanii katika mkataba huo.
Sasa hapo unakuwa unajiuliza, kwa nini kweli TFF baada ya
usuluhishi walishindwa kuweka hayo hadharani? Ukimya wao unalenga au
unamaanisha nini? Bado majibu hakuna.
Simba wanaibua hoja nyingine, hata maofisa walioingia kusikiliza
kesi yao na Messi, licha ya kuwa ni TFF lakini wote watatu kutoka katika
shirikisho hilo walikuwa Yanga, hivyo wanahisi kuna mchezo wanachezewa.
Inawezekana kukawa na ukweli au ni hisia tu! Yote mawili
yanawezekana lakini kukosekana kwa uwazi katika suala hilo ndiyo chanzo kikubwa
cha mkanganyiko mkubwa uliojitokeza.
Binafsi nao sakata hilo ambalo inaonekana kweli kuna mkanganyiko
usio na sababu, limetokea katika wakati mwafaka kabisa.
Angalia kwenye vyombo vingi vya habari, utaona ni picha za wachezaji mbalimbali wanaojiunga
na timu mpya katika Ligi Kuu Bara.
Hiki ndiyo kipindi cha usajili, kipindi ambacho alipitia Messi kwa
furaha lakini sasa yuko katika malumbano. Wachezaji wengi wanakuwa kama wendawazimu
wakati wa kipindi hiki.
Moja ni hamu kubwa ya kusajiliwa na timu fulani na akiipata,
anakuwa kama amewehuka. Pili ni suala la fedha, wapo ambao wamekuwa wakipata
fedha ambazo hawakuwahi kuzishika au kuzitegemea. Baada ya hapo, wazimu wa
furaha na faraja ya alichokipata, unamfanya asahau kabisa suala la mkataba.
Wako ambao kwa ajili ya haraka hawataki hata kuisoma mikataba yao.
Tena wanaona wanacheleweshwa na wanachoona ni muhimu wakati huo ni kuisaini tu
na si vinginevyo.
Baada ya fedha kwisha, pia kuzoea kwamba sasa ni mchezaji wa timu
fulani, macho yanafunguka upya na anaanza kukumbuka sasa kuusoma mkataba ambao
alisaini mwaka au miaka miwili iliyopita. Hii ndiyo njia aliyopitia Messi.
Yeye kutokuwa na mkataba ni kosa lake, wengi wamekuwa wakikwepa kumueleza
hilo lakini alistahili kuwa na mkataba wake. Simba huenda tunaweza kuwapa kosa
kwa kushindwa kuonyesha uungwana na kumkumbusha, kama walimpa akautupa, basi
hilo ni tatizo lake.
Wachezaji wanaosaini sasa wameliona hili la Messi? Je,
limewasaidia kuisoma vizuri mikataba yao pamoja na vipengele vya kuvunja wakiwa
wameamua kufanya hivyo au pale klabu inapoamua kuwaacha?
Wana uhakika wana mikataba orijino? Je, inalingana na ile ya klabu
ambayo inakuwa mitatu. Mmoja wa mchezaji, mmoja wa klabu na wa mwisho wa TFF?
Hivyo, lazima kuwe na umakini, ikiwezekana hata waikabidhi kwa
wataalamu kama wanasheria ili wawasomee na kupata uhakika wa mambo.
Haraka ya kutaka kumalizana na timu fulani au haraka ya kupata
fedha za usajili, ndiyo tatizo kubwa linalowatafuna wachezaji. Vema wakajiamini
na kuwa watulivu kwa kuwa mkataba wa kazi ndiyo mwongozo wa muda wote wa ajira.
Ukiyumba na kupotea, basi umejipoteza kwa muda wote wa kipindi cha
kuwa kazini, iwe mwaka, miaka miwili, mitatu au zaidi. Lazima tukubali, kukiwa
na umakini wakati wa kuingia mikataba, basi mwisho hakuna tatizo tena litakalojitokeza.
Alichokosea Messi au walichokikosea Simba hakipaswi kurudiwa na
wengine. Ndiyo maana nimewakumbusha kwamba kinachotokea sasa kwa Messi na
Simba, si sinema tu, ni shule kwenu.







Saleh ulituonyesha katika mkataba wa Simba na Messi kipengele kinachosema 'mchezaji chini ya umri wa miaka 18 hataruhusiwa kusaini mkataba wa miaka mitatu'.Swadakta,sasa mbona Simba imemsainisha huyo Singano miaka mitatu wakati akiwa na umri wa miaka 17?Uoni hicho ndicho kipengele ndicho kilichofanya mkataba kuchakachuliwa?
ReplyDelete