Kikosi cha Simba, jana Jumanne kilianza mazoezi yake ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ikiwa ni siku moja tu tangu wamtangaze kocha wao mpya, Muingereza, Dylan Kerr anayetarajiwa kuwasili nchini wikiendi hii.
Simba ambayo msimu uliopita wa ligi ilimaliza nafasi ya tatu, imeanza mazoezi ya gym chini ya kocha wao msaidizi, Seleman Matola, huku ikiwa na wachezaji wachache kutokana na wengine kuwa mbali na Dar ambapo mazoezi hayo yatadumu mpaka hapo atakapowasili kocha mkuu.
Matola amesema kuwa jana Jumanne kikosi hicho kilianza mazoezi yake ya kujiwinda kwa msimu wa ligi kuu rasmi kwa kuanzia gym ambapo watadumu katika mazoezi hayo mpaka watakapoingia kambini rasmi.
“Ndiyo tumeanza mazoezi kidogokidogo ya gym ambapo tutakuwa tukifanya kila siku asubuhi kwenye gym iliyopo Chang’ombe tukisubiri kuingia kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
“Ingawa tumeanza mazoezi lakini idadi ya wachezaji ni ndogo kutokana na wachezaji wengi kuwa mbali na hapa Dar, lakini mpaka wiki ijayo watakuwa wamesharejea kwani kambi rasmi ndiyo itakuwa inaanza,” alisema Matola.
0 COMMENTS:
Post a Comment