Na
Saleh Ally
NIMEWASIKIA
watu wengi wakitoa maoni yao kuhusiana na kujiuzulu kwa Rais wa Shirikisho la
Soka la Kimataifa (Fifa), Joseph ‘Sepp’ Blatter.
Blatter,
raia wa Uswisi, ameamua kuachia ngazi baada ya kuwa kwenye usukani kwa miaka
17, tena akiwa ameshinda mara nyingine, lakini kashfa ya rushwa imemuondoa.
Wakati
Blatter anaondoka, kila mmoja anaweza kusema lake na huenda wengine wakaingiza
ushabiki wakiona ulikuwa ni utawala wa muda mrefu na alistahili kuondoka.
Nilivyoona,
wengi walifananisha uongozi wa Fifa na uongozi wa nchi, kwamba kuna mhula wa
kwanza na wa pili kama ambavyo sasa Rais Pierre Nkurunziza anavyopata wakati
mgumu kutokana na kutangaza kugombea muhula wa tatu.
Blatter
ameondoka lakini si kwa faida ya Afrika wala Tanzania, Blatter ameondoka kwa
kuwa Marekani, Uingereza na Ufaransa hawamtaki na siku zote wamekuwa wazi
katika hilo.
Mataifa
hayo makubwa matatu, yameungana. Awali walikuwa Waingereza, Ufaransa nao
wakaingia lakini safari hii wakatumia kigezo cha zile fedha za rushwa
zilizopitia Marekani na Shirika la Kijasusi la FBI, likawa na nafasi ya
kuingia.
Mkurugenzi
wa FBI, James Comey amesema wazi, kwamba hata ingekuwa senti lakini kama fedha
hiyo imegusa katika anga za Marekani, basi inawahusu.
Jibu
lake lilitokana na maswali mengi, kwamba hawa Marekani ambao mpira kwao ndiyo
unaanza kuingia, tena hawaupendi kihivyo, vipi leo wavalie njuga suala la
rushwa Fifa?
Bado
kuna ishu ya michuano ya Kombe la Dunia, mwaka 2018 nchini Urusi na 2022 kule
Qatar. Waingereza, hawakufurahia. Ufaransa pia wanaona si sawa, lakini
Wamarekani walijaribu, wakapigwa chini pia na 2018 imekwenda kwa wapinzani wao
wakubwa kisiasa.
Mataifa
hayo makubwa yamejaribu hata kukumbushia Kombe la Dunia mwaka 2010 ambalo
lilifanyika kwa mara ya kwanza Afrika. England ilikuwa nchi iliyopinga kweli
kwa madai bado bara hili halijafikia kuandaa michuano hiyo mikubwa, kisingizio
kingine ni usalama mdogo wa Johannesburg na miji mingine ya nchi hiyo.
Kombe
la Dunia lilifanyika bomba sana, naweza kuwa shahidi maana nilikaa Afrika
Kusini mwanzo hadi mwisho nikitembea katika miji ya Johannesburg, Cape Town,
Darbun na mingine mingi, wezi walikwenda likizo, wakatulia kushuhudia boli,
England wakawa kimya.
Ukiangalia
michuano sita ya Kombe la Dunia, Ulaya imepewa mara mbili. Anzia mwaka 2002
(Asia), 2006 (Ulaya), 2010 (Afrika), 2014 (Amerika Kusini), 2018 (Ulaya) na
2022 (Asia).
Utaona
katika hizo mara sita, Ulaya ya Kati na Magharibi imepata mara moja wakati
Ujerumani ilipoandaa mwaka 2006. Baada ya hapo ni Afrika, Amerika Kusini, Ulaya
Mashariki na Asia tena.
Waingereza
wanaona wanadharauliwa, Wafaransa wameshawishika na sasa Wamarekani wameingia
na hakuna ubishi, Blatter na Fifa yake, kweli watakuwa wanakula rushwa, lakini
kero ya kuona hawapewi nafasi ya ukubwa walionao, sasa wameamua kuuonyesha.
Mimi
sina haja ya kuangalia nchi ipi imepewa, ninachoangalia Tanzania inapata nini.
Tumeona Blatter alivyosukuma mabilioni ya dola kuja Afrika. Amefanya hivyo ili
afaidike na kura wakati wa uchaguzi kutoka Afrika (Caf) na Asia (AFC).
Kweli
mabara haya mawili ndiyo yanayoongoza kumuunga mkono yakifuatiwa na Amerika
Kusini. Blatter anafaidika, nayo yanafaidika. Kusherehekea kuondoka kwa Blatter
ambaye sasa anaondoka na vazi lililokuwa linatusitiri ni kushabikia
usichokijua.
Kamwe
sitaki kushabikia Umarekani wala Uingereza kwa kuwa mimi ni Mtanzania nisiye na
nyumbani kwingine. Bado sijui anayekuja kuchukua usukani kwa kuwa hali halisi
inaonyesha Wazungu watageuka na ikiwezekana hatakuwa Prince Ali wa Jordan,
badala yake wataangalia Mzungu mwenzao kama Luis Figo au Michel Platini ambaye
wanaamini atawaunga mkono.
Simlilii
Blatter na kuondoka kwake, kama alifanya makosa, kweli anastahili kuyatumikia,
lakini wanaohakikisha anaondoka kwa maslahi yao, unafikiri watajali maslahi ya
Tanzania? Hii ndiyo hofu yangu.
Kwamba
gwiji huyo alikuwa na makosa yake, lakini Tanzania imefaidika na viwanja vya
nyasi, kozi za makocha, waamuzi na hata fedha. Kama hazikuwa na faida labda
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), halikuzitendea haki kwa ajili ya maendeleo.
Baada
ya Blatter, Mzungu anayekuja kweli ataikumbuka Tanzania? Nchi inayobaki ilipo
kila siku katika soka? Tena ukiangalia, tayari Wazungu wameshaanza kuzungumzia
ukubwa wao, sisi Tanzania tu wachanga kila kukicha! Eeh Blatter, nenda babu,
ila siku itafika, watakukumbuka tu.
Kaka ni kilio tuu kwa Afrika,yaani hawa wazungu mwisho watapanga utaratibu wa waafrika wangapi wanatakiwa kucheza Ulaya.
ReplyDelete