Kiungo mpya wa Azam FC, Mnyarwanda, Jean Baptiste Mugiraneza, anatarajia kutua nchini
leo Jumatano na kufanyiwa vipimo kisha kufanyiwa majaribio kama ilivyo kwa kipa
mpya wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Vincent Atchouailou de Paul Angban.
Azam tayari ina wachezaji wa kigeni watano na imebakiza nafasi
mbili pekee kuweza kukamilisha wachezaji wa kimataifa saba ndani ya klabu hiyo
na kwa sasa imealika wachezaji watano wa kigeni kufanya majaribio ndani ya
klabu hiyo lakini mpaka sasa amewasili kipa huyo pekee.
Ofisa habari wa timu hiyo,
Jaffar Idd, alisema kwa sasa wapo kwenye maandalizi na kuangalia wachezaji
wapya wa kimataifa ambao wametua klabuni hapo kwa ajili ya majaribio.
Idd alisema kuwa, wanafanya
maandalizi ya nguvu na kuangalia uwezo wa wachezaji wao kutumia michezo ya
kirafiki kabla ya kuanza michuano ya Kombe la Kagame mapema wiki ijayo.
“Wachezaji wa kimataifa tumewaalika watano kwa ajili ya majaribio
hapa klabuni na mpaka sasa amefika yule kipa raia wa Ivory Coast, hao wengine
wataendelea kuja kuungana na timu kwa kuangalia uwezo.
“Lakini wanapotua ndani ya timu, lazima wafanye majaribio kwanza
na kama tutaridhika nao ndipo tunaweza kuwapa mikataba na kocha ndiye mwenye
nafasi ya kuangalia anahitaji mchezaji wa aina gani na kama ameridhika na
kiwango,” alisema Idd.
Kwa upande mwingine, mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, alisema kuwa
kiungo Mnyarwanda anatarajia kutua nchini leo Jumatano.
“Mugiraneza anatarajiwa kutua leo na atafanyiwa vipimo na kuungana
na wenzake kufanya majaribio kisha baada ya hapo mambo yote yatawekwa hadharani,
maana mazungumzo ya awali yalishafanyika,” alisema kiongozi huyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment