Kocha mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, anatarajia kutumia
mbinu mpya ndani ya kikosi hicho kwa kuwafanyisha wachezaji wake mazoezi matupu
bila ya kugusa wala kuchezea mpira katika kambi ya timu hiyo iliyopo wilayani
Lushoto mkoani Tanga.
Kikosi hicho cha Simba kimeenda kujichimbia Lushoto kwa ajili ya
kuweka kambi yake ya wiki mbili ya kujiandaa na michezo ya ligi kuu kwa msimu
ujao.
Kerr alisema kuwa katika kambi hiyo, ameandaa programu maalumu ya
kuwajenga kimwili pamoja na kuwafanya wachezaji wake kuwa na nguvu
watakapopambana na wachezaji wa timu pinzani ambapo katika programu hiyo,
kutakuwa hakuna kuchezea mpira hata kidogo.
“Katika kambi ya huku Lushoto, nimeandaa programu maalum ya
kuwajenga na kuwafanya wachezaji wawe fiti ambapo katika mazoezi tutakayokuwa
tunafanya kila siku, hatutakuwa tunagusa mpira.
“Lengo kubwa la programu hiyo ni kutaka kuwafanya wachezaji wawe
imara hata pale watakapokutana na wapinzani ambao watakuwa wapo imara zaidi
yetu na katika hilo, nitashirikiana na kocha wangu wa viungo, Dusan Momcilovic.
“Nimeona niwape wachezaji mazoezi hayo baada ya kuona wengi wao
hawapo katika kiwango kizuri cha ‘fitness’ ambacho mchezaji yeyote yule
anatakiwa kuwa nacho,” alisema Kerr ambaye aliwahi kuichezea Reading ya
England.
0 COMMENTS:
Post a Comment