Miaka mitatu sasa, Simba haijafuzu kushiriki michuano ya kimataifa
inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf), hiyo haimsumbui straika mpya
aliyerejea kikosini, Mussa Mgosi ambaye amewataka mashabiki kutulia kwani hali
hiyo itarejea ndani ya msimu huu.
Mgosi aliyejiunga na Simba siku chache zilizopita baada ya
kumaliza mkataba na Mtibwa Sugar, amesema: “Heshima
iliyopotea Simba, sasa itarudi.”
Alisema kwa kushirikiana na wenzake, atahakikisha msimu ujao
watafanya kila liwezekanalo ili Simba kama siyo kutwaa ubingwa basi ishike
nafasi ya pili na kukata tiketi ya kucheza michuano ya Caf.
“Nimetoa kauli hiyo kwa kuzingatia usajili uliofanywa kwa maana
wale tunaojiunga na timu tukishirikiana na wenzetu tuliowakuta hapo tutakuwa na
timu bora,” alisema Mgosi.
“Sasa ndiyo muda wa Simba
kurudisha heshima yake kama zamani kwani imedharaulika kwa muda mrefu lakini
napenda kusema msimu uliopita ndiyo ulikuwa mwisho wa dharau hizo.”
Mbali na Mgosi, wachezaji wengine waliosajiliwa na Simba hadi sasa
ni kiungo Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City, Mohammed Fakhi (KMKM), Samih Ali
Nuhu (Azam FC), Laudit Mavugo na Nimubona Emiry (Vital’O) na kiungo Emmanuel
Ntinde kutoka Burkina Faso ya Morogoro.
0 COMMENTS:
Post a Comment