July 3, 2015

KAPOMBE

Na Saleh Ally
UMESIKIA ule mjadala wa kuongezwa kwa wachezaji saba wa kigeni ambavyo umekuwa ukiendelea kutoka kila upande.

Tayari kuna makundi mawili, moja linaunga mkono kuongezwa kwa idadi hiyo ya wachezaji kutoka watano hadi saba. Maana yake wameongezwa wawili badala ya kupunguzwa wawili.


Wakati wa uongozi wa Leodegar Tenga, TFF ilipunguza wachezaji kutoka kutoka 10 hadi watano. Halafu ikaahidi itapunguza hadi wafike watatu tu na hakutakuwa na kipa kutoka nje ya Tanzania.

Uongozi wa Jamal Malinzi ukaamua kuongeza hadi wafikie saba. Hii ni baada ya Yanga, Azam FC kuonyesha wanahitaji sana hilo kwa madai kwamba watawasaidia katika michuano ya kimataifa. Simba ni kati ya waliowaunga mkono.
 
SIMBAKuongezwa tena kwa wachezaji hao kumezua mdahalo, ninaamini hata wangebaki vilevile au kupunguzwa, bado mjadala ungeendelea.

Kwangu kama nilivyosema awali, nataka kujifunza na sasa nafuatilia kwa karibu kuona kama tumefaidika au la lakini hoja yangu ni tofauti kabisa.

Hawa wachezaji wa nyumbani ambao tumekuwa tukiwatetea kwamba kuwajazia wageni ni kuwaua. Wao wanafikiria nini na kwa nini tunataka kuwapa malezi ya “Watoto wa mama”, yaani wapo tu, hawataki kuonyesha nia ya ushindani na kufika mbali.


Hawa wachezaji wa ndani, wanaonekana kutetewa kwa kuwa wageni wengi watawamaliza. Vipi wanashindwa kushindana na hao wageni na kwa nini wanahofia sana changamoto yoyote.
Wako nyumbani ni waoga, wanapendwa kutetewa, sisi tunawaonea huruma lakini wachache kati yao wako tayari kupambana na wageni.
SIMBA
Mfano mzuri ni Simon Msuva, amekuwa mfungaji bora na wageni wapo. Samuel Kamuntu na Rashid Mandawa wameonyesha uwezo na kufunga mabao mengi licha ya kuwa katika timu ndogo. Hawa wanaweza kuwa mfano wa wenyeji kupambana na changamoto ili kuinua ubora wao.

Ukiachana na kuendelea kubaki nyumbani ili wapambane, ninahoji vipi wachezaji wa Tanzania hawataki au hawajiamini kwenda kucheza nje ya nchi yetu mfano nchi za jirani tu kama Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na kwingineko.

Kila anayecheza, msimu mmoja anataka kurejea nyumbani lakini wageni kila siku wanatamani kuja kucheza hapa kwetu na baadaye wanafanikiwa.

Haruna Niyonzima alikuwa kipenzi cha mashabiki na viongozi wa APR, lakini alilazimisha kuondoka Rwanda kwa kuwa alitaka changamoto mpya. Leo anaonekana ni bora, amejifunza mengi na maslahi yake yako juu kuliko wachezaji wa Tanzania!

Unaweza kusema nje kunahitaji uzoefu sana, kunatakiwa mchezaji aliyekomaa kiushindani kama ilivyo kwa Mrisho Ngassa. Mimi nitakuambia hata yeye alikuwa na ugonjwa huo wa uoga na ameondoka amechelewa sana, jambo ambalo naona hana nafasi kubwa ya kucheza kipindi kirefu, naye atarudi nyumbani. Utaona!
 
MBEYA CITYSi lazima uzoefu, uwezo, kipaji alichonacho mchezaji, nia ya kutaka kutokana na kushindana na kushinda, vinatosha kuweka kwenye begi na kuanza safari ya kwenda kupambana na changamoto za ugenini.

 Mfano wangu mzuri ni kwa Mbwana Samatta aling’ara na Mbagala Market ikiwa daraja la kwanza.

Akachukuliwa na Simba, aliichezea kwa nusu msimu tu akaondoka kwenda TP Mazembe na sasa ni staa Afrika. Uzoefu upi aliupata hata kwenye Ligi Kuu Bara, hakucheza hata mechi 20!

Thomas Ulimwengu, alicheza Moro United akiwa mmoja wa wachezaji kinda katika kituo maalum cha kulelea vijana. Naye hafikishi hata mechi 10 za Ligi Kuu Bara, amekwenda TP Mazembe, anafanya vizuri na anajulikana Afrika.

Sasa hawa wanaong’ang’ania kubaki hapa, tena wengine wamekuwa wakipata bahati wamekuwa wakikataa huenda kwa kuwa wamezoea kuonekana mastaa kwa mashabiki wa Yanga na Simba ambao wakati mwingine wamekuwa wakiwatuza fedha utafikiri wako kwenye muziki!

Wako wamekuwa wakilipiwa kodi na mashabiki au wanachama wa klabu zao. Wamekuwa wakiwekewa mafuta kwenye magari yao na hata kulipiwa gharama nyingine za maisha. Hilo ni jambo la hovyo kabisa na huenda ni kati ya mambo ya kijinga yanayowalemaza na kuwafanya wazidi kupenda nafuu na kung’ang’ania kucheza nyumbani huku wakilalama eti wageni ni wengi.

Wote tumekuwa tukikubaliana kwamba umefika wakati Tanzania inahitaji wachezaji zaidi ya 10 wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania ambao watakuwa wanakuja na mawazo tofauti ili kujenga kikosi bora na imara cha timu ya taifa.

 Vipi wachezaji kama Frank Domayo, Shomari Kapombe, Kelvin Yondani, Ramadhani Kessy, Salum Telela na wengine wengi wako hapa nyumbani hadi leo? Wamewahi lini kujaribu angalau kusambaza wasifu wao kwa timu mbalimbali kuonyesha wana nia? wanataka watafutwe tu?

Mchango wa Ulimwengu na Samatta umekuwa ukionekana lakini lazima tukubali wao pekee hawatoshi, lazima waongezeke na hawataongezeka kutokea peponi. Hadi wachezaji walioko nyumbani watakapobadili mawazo na kuamini wana safari ndefu kwa ajili yao na taifa lao na kuachana na tabia ya utoto wa mama kung’ang’ania kucheza soka nyumbani.

Unaweza kuwatetea kwamba hawapati nafasi, lakini tuna mifano mingi ya wachezaji waliokwenda kucheza nje, mfano Sweden, Ufaransa, Ujerumani lakini wakarejea nyumbani wakiwa wamejazwa ujinga na viongozi wa Yanga na Simba ambao waliwataka warejee na mwisho wote leo hawako katika timu hizo.
 
STAND UNITEDKwangu ninawaona ni wao, wenye madeko, wasio watu wa kujituma, wasiojitambua na wanaosubiri majuto wabaki kusema najua “ninge…ninge” ambayo kamwe haitabadilika na umri hautarudi nyuma, mwisho watabaki kuwa watu wa kulaumu huku wakiwa wamesahau wao ndiyo tatizo namba moja.


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic