IKIWA inaongoza kundi A kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kukusanya pointi sita, Simba imeweka wazi vikwazo vitakavyofanya mchezo huo kuwa mgumu.
Leo imetia kambi nchini Sudan ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wao dhidi ya Al Merrikh unaotarajiwa kuchezwa Machi 6.
Seleman Matola, kocha msaidizi wa Simba amesema kuwa kupoteza kwa mechi zao mbili pamoja na Gomes kuwa ndani ya Simba ni miongoni mwa sababu ambazo zitaongeza ugumu kwenye mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
"Tunakutana na wapinzani ambao hawana cha kupoteza kwa kuwa wametoka kupoteza mechi zao zote mbili. Wao hawana presha tofauti na sisi ambao tuna pointi na tunahitaji kushinda.
"Pia tukumbuke kwamba Al Merrikh wanatambua kwamba mwalimu wetu Didier Gomes alikuwa ndani ya kikosi hicho na aliamua kuondoka mwenyewe hivyo itakuwa na presha kubwa kwao kutaka kushinda.
"Wanahitaji kulipa kisasi kwa mwalimu wao kuondoka kwa kuwa walikuwa wanamhitaji ila yeye mwenyewe aliondoka na kuja ndani ya Simba, wengi wanafikira kwamba itakuwa kazi nyepesi, hakuna kitu kama hicho.
"Yote kwa yote tumejipanga ili kuona kwamba tunapata matokeo chanya kwani ushindani tunajua upo nasi pia tutashindana ndani ya uwanja, mashabiki waendelee kutuombea dua,"
Gomes aliibuka ndani ya Simba kurithi mikoba ya Sven Vandenbroeck ambaye alibwaga manyanga mapema mwezi Januari na sasa yupo zake nchini Morocco.
0 COMMENTS:
Post a Comment