August 14, 2015


Ikijiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya URA, Simba imehamia Uwanja wa Chuo Kikuu cha Polisi, Kurasini jijini Dar es Salaam uliokuwa unatumiwa na Yanga.


Kabla ya hapo, Simba ilikuwa ikitumia Uwanja wa TCC Chang'ombe jijini Dar pia. Simba haina uwanja wa mazoezi na miaka yote imekuwa ikiishi maisha ya kuhamahama uwanja mmoja kwenda mwingine kama ilivyo kwa ndugu zao Yanga ambao wana uwanja pale kwao Kaunda, lakini nao uko hovyo ile mbaya.

Yanga pia ilikuwa ikiutumia uwanja huo unaomilikiwa na Jeshi la Polisi nchini kwa ajili ya michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni, ambapo Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm na benchi lake la ufundi, walikuwa wakifanya mazoezi kwa kificho kwa kutotaka mashabiki wala waandishi wa habari.

Ofisa Michezo wa Chuo Kikuu cha Polisi ambaye pia ni Msaidizi wa Ulinzi wa TFF anayetambulika na Fifa, Mohamed Manyai, alisema kuwa timu hiyo imeomba kutumia uwanja huo kwa siku tatu pekee.

Manyai alisema siku hizo walizoziomba maalum kwa ajili ya matayarisho ya mechi ya kirafiki dhidi ya URA, ndipo uongozi ukawaruhusu kuutumia uwanja huo.

Aliongeza kuwa, uwanja huo walianza kuutumia juzi Jumatano jioni kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 12:00 jioni, kabla ya kumaliza leo Ijumaa ambayo ni siku ya mwisho kufanya mazoezi uwanjani hapo.


“Walitimiza masharti yote ya uombaji wa uwanja huo, kama uongozi wa polisi tumewaruhusu kuutumia uwanja huo kwa siku tatu walizoziomba,” alisema Manyai.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic