August 14, 2015


Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr, ametamka kuwa kati ya nafasi zinazompa changamoto ya upangaji wa timu, basi ni safu ya kiungo yenye viungo nane.


Safu hiyo ya kiungo inachezwa na Jonas Mkude, Abdi Banda, Peter Mwalyanzi, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto, Justice Majabvi, Awadh Juma na Ibrahim Ajibu.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya SC Villa ya Uganda uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambao ulimalizika kwa Simba kushinda bao 1-0.

Kerr amesema anafurahia kuwa na viungo wote hao wenye uwezo mkubwa hali inayosababisha apate ugumu wa kupanga kikosi cha kwanza.

Kerr alisema hana hofu juu ya safu ya kiungo kutokana na kila mmoja atakayempa nafasi ya kucheza anaonyesha kiwango kikubwa, tofauti na safu ya ushambuliaji ambayo inahitaji maboresho kidogo.

Aliongeza kuwa, kila kiungo ana nafasi yake ya kucheza kwenye kikosi chake kutokana na aina ya mechi atakayokutana nayo kwenye siku husika.

“Kati ya nafasi ambazo zinanipa ugumu wa kupanga namba kwenye kikosi changu, basi ni safu ya kiungo yenye wachezaji nane ambao wote wana uwezo wa kucheza soka safi.

“Kiukweli kabisa nakabiriwa na changamoto kubwa ya kuwapanga viungo hao, lakini kila mmoja nitampanga kutokana na aina ya mechi nitakayoicheza, nikiamini nikimtumia ataonyesha kiwango kikubwa.


“Ukiwa na idadi kubwa ya wachezaji na wote wenye uwezo mkubwa, ushindani unaongezeka katika timu kutokana na kila mmoja kuonyesha uwezo mkubwa ili apate nafasi ya kucheza,” alisema Kerr.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic