Ile ishu ya Simba kumleta kipa kutoka
nchini Brazil, Ricardo Andrade limeyeyuka juu kwa juu sababu kubwa ni uongozi
wa timu hiyo kunasa saini ya Muivory Coast, Vincent Agban.
Simba ilikuwa mbioni kumleta nchini Andrade kwa
ajili ya kuzungumza naye na kumpa kandarasi kwa ajili ya msimu ujao baada ya
kumfanyia majaribio lakini ghafla mpango umegeuka baada ya kuridhishwa na uwezo
wa Agban na kumpa mkataba wa miaka miwili.
Awali, Wekundu hao walikuwa na hesabu ya
kumuongezea mkataba kipa wao, Ivo Mapunda kisha wamsainishe Mbrazili huyo kwa
ajili ya kusaidiana na kipa mwingine kinda, Peter Manyika kwenye Ligi Kuu Bara
msimu ujao.
Baada ya kutoelewana na Ivo, ndipo wakaamua
kumsainisha Agban na kumtosa Andrade kwa kigezo kuwa haiwezekani nafasi ya kipa
ikawa na maprofesheno wawili. Hata hivyo, Rais wa Simba Evans Aveva alisema jana wanatarajia kumalizana na Ivo Mapunda ndani ya siku mbili.
Aidha, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya
Simba, Kassim Dewji, amesema nafasi ya kipa wa tatu, atasajiliwa kipa kutoka
Tanzania na tayari wapo sokoni kuangalia atakayewasaidia msimu ujao.
“Agban anatosha, atakuwa na Manyika na
watasaidiana na kipa mwingine ambaye tutamsajili kutoka hapahapa Tanzania,”
alisema Dewji.
Simba sasa ina wachezaji wa kigeni sita kati ya
saba kulingana na kanuni za ligi kuu, wengine ni Waganda, Hamis Kiiza, Juuko
Murshid, Simon Sserunkuma, Mzimbabwe, Justice Majabvi na Mrundi, Emiry
Nimubona.
0 COMMENTS:
Post a Comment