September 21, 2015


Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga, Donald Ngoma amefanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi zake tatu za kwanza za Ligi Kuu Tanzania Bara.


Ngoma raia wa Zimbabwe alianza kuifungia Yanga bao katika mechi ya ufunguzi wa ligi wakati iliposhinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Bao hilo lilionekana ni kama kuondoa ‘nuksi’ kwa kuwa katika mechi za kirafiki, mambo yalionekana kutokuwa mazuri kwa Mzimbabwe huyo, hadi baadhi ya wadau wakaamini Yanga ilikuwa imeingizwa mkenge.

Mechi iliyofuata, Yanga ilishinda kwa mabao 3-0 dhidi ya timu ngumu ya Prisons. Ngoma alikuwa ‘ubaoni’ tena baada ya kufunga bao moja, safari hii akafikisha mabao mawili.

Swali likawa kweli ataweza kufikisha mabao matatu katika mechi tatu kwa kuwa ilikuwa inafuatia JKT Ruvu iliyokuwa imetoka kujeruhiwa. Ngoma akatoa jibu kwa kufunga bao safi kabisa na kuweka hesabu ya mabao matatu katika mechi tatu sawa na Amissi Tambwe.

Ngoma sasa ana mabao matatu sawa na mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora msimu mmoja kabla ya msimu uliopita. Lakini akashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 14 msimu uliopita.

Ngoma kwake ndiyo msimu wa kwanza akicheza Ligi Kuu Bara na amefanikiwa kufunga mabao matatu katika mechi tatu. Jambo zuri kwa Yanga au kamati yake iliyohusika na usajili inaonekana ililenga au kusajili mchezaji sahihi kwa kuwa kazi yake ni kufunga na anaonyesha kweli anaweza.

Si sahihi kuanza kumtwisha Ngoma misifa kwa wingi kwa sasa, kwamba hakuna kama yeye au hashikiki hadi hapo atakapofanya mambo mawili.


Nianze na yale aliyoyafanya kabla ya kwenda kwenye namna gani tunaweza kuthibitisha. Ngoma amefunga mabao matatu lakini mawili ni ya aina yake na yanayoweza kufungwa na mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa, hilo halina ubishi.

Bao lake la kwanza, mechi dhidi ya Coastal Union, Ngoma alifunga bao katikati ya mabeki wanne wa Wagosi wa Kaya, akionyesha namna gani alivyotulia. Lakini alimsubiri kipa kabla ya kupiga upande mmoja aliotokea kipa na asingeweza kugeuka.

Bao lake linaloweza pia kuingia kwenye moja ya mabao bora ya Ligi Kuu Bara, ni lile la tatu alilofunga dhidi ya JKT. Kwani alianzia na mpira mbali akitoa pasi na kuomba, akatoa na kuikuta tena kabla ya kufunga kwa mchomo safi wa chini ulioonekana ana malengo na huenda ni vigumu kuona wachezaji wengi hapa nyumbani wakifunga hivyo.

Uthibitisho kwamba kweli Ngoma ni bora na anaweza kuwa bora zaidi ni kama atafunga au kusababisha bao katika mechi dhidi ya Simba wiki ijayo. Mechi yenye presha kubwa, mechi ambayo mchezaji bora anaweza kuonekana hana lolote.

Kuhimili presha ni sehemu ya kipimo cha kuonyesha ubora wa mchezaji fulani ana uwezo, mzoefu ana msaada na pia ana uwezo. Pili, tusubiri atakapokwenda kucheza mikoani ambako viwanja vingine mchezaji analazimika kuutuliza mpira mara sita, saba.



Kama Ngoma ataifunga Simba, akaondoka na Yanga kwenda mikoani akaifungia pia, basi kuna kila sababu kuwa kweli ni mchezaji ambaye Watanzania wangependa kuona anasajiliwa na timu za hapa nyumbani.

Lengo la usajili ni kuona kunakuwa na wachezaji wanaoashiria ushindani, upinzani ambao utajenga na kufanya mchezo wa soka nchini kusonga mbele. Acha tuendelee kuona ngoma ya Ngoma inavyokuwa.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic