Zikiwa zimebaki takribani siku nne kabla
ya timu ya Simba kucheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara, msimu huu
dhidi ya African Sports, kocha mkuu wa kikosi hicho, Muingereza, Dylan Kerr,
ameibuka na kuwataka wachezaji pamoja na mashabiki wa timu hiyo kuwa kitu
kimoja kwa sasa.
Simba itaanza msimu kwa kucheza ugenini
huko mkoani Tanga, ambapo katika kujiandaa na mchezo huo bado ipo visiwani
Zanzibar ikimalizia maandalizi ya mwisho-mwisho huku kikosi hicho kikionekana
kuwa imara kila kukicha.
Katika kuhakikisha kikosi hicho kinapata
ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza, tayari kocha huyo wikiendi iliyopita
alikuwa mkoani Tanga na kuishuhudia African Sports ikichapwa na Coastal Union
bao 1-0, katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani ambao
Jumapili hii ndiyo watautumia.
Licha ya kuwashuhudia wapinzani wake,
lakini hakuwa tayari kusema lolote zaidi ya kusema watu wasubiri siku ya mechi
ndiyo wataona mziki wao.
“Kuelekea kuanza kwa ligi, nawaomba
mashabiki na wachezaji wa Simba kujivunia kuwa ni Wanasimba, hivyo wanatakiwa
kujitoa kwa nguvu zao zote kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri katika kila
mchezo na hilo linawezekana kama kweli tutaamua mashabiki waje uwanjani
wikiendi ijayo wakaone kazi tutakayofanya,” alisema Kerr.
0 COMMENTS:
Post a Comment