Licha ya Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza, Stewart Hall, kuibuka na
ushindi kwenye michezo yake minne mfululizo ya Ligi Kuu Bara, bado amekiri kuwa
hafurahishwi na maamuzi yanayotokea kwenye mechi hizo.
Kocha huyo amefunguka kuwa, mara kadhaa amekuwa haridhishwi na
waamuzi wa ligi hiyo, lakini ameamua kuweka wazi baada ya maamuzi mabovu zaidi
yaliyofanywa kwenye michezo yake miwili ya mwisho dhidi ya Mwadui FC
waliyoshinda 1-0 na wa Mbeya City waliyoshinda 2-1.
Stewart alifika mbali na kusema kuwa muda mwingine huwa anafikiria
labda waamuzi hawapendi kuona Azam inafanya vizuri, ndiyo maana yanatokea yote
hayo na maamuzi yasiyo na haki kwenye mechi zao.
“Waamuzi wamekuwa tatizo sana, kadi nyingi hutolewa hovyo kwenye
mechi zetu lakini pia haki imekuwa haipatikani. Ishu si kushinda mechi
mfululizo, kinachotakiwa ni mpira wa haki na kuchezesha mechi kwa kufuata
sheria na si vinginevyo.
“Kuna muda mtu unaweza kufikiri labda watu hawataki kuona Azam
inafanya vizuri kwenye ligi, maana haiwezekani kwenye mechi mbili za mwisho
mambo yaende tofauti kabisa, hili si zuri kwa kweli, inabidi tubadilike kwa
ajili ya amani na maendeleo ya soka,” alisema Stewart.
Baada ya raundi nne za ligi, Azam inashikilia nafasi ya pili ikiwa
na pointi 12, sawa na Mtibwa Sugar walio nafasi ya tatu pamoja na vinara Yanga
SC.
0 COMMENTS:
Post a Comment