Baada ya kushushiwa shutuma nzito juu ya maamuzi yake katika mechi
ya Simba dhidi ya Yanga, mwamuzi, Israel Nkongo ameibuka na kuwataka wanaoona
hawakutendewa haki waweze kufika kwenye vyombo husika na kumshitaki ikiwemo
kwenye Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Simba imekuwa ikilalama kuhusiana na kukandamizwa na Nkongo katika
mechi hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, wikiendi iliyopita na
kufungwa mabao 2-0, huku Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara akithibitisha kuwa
tayari jana wamewasilisha barua yao ya malalamiko kwenye Shirikisho la Soka la
Tanzania (TFF).
Nkongo
amefunguka kuwa kwa upande wake kanuni zinambana kuzungumzia mechi alizowahi kuwa
mwamuzi, lakini kama timu yoyote itaona imeonewa na haikutendewa haki, basi
inaweza kufuata ngazi muhimu na kumshitaki kwenye sehemu anazoweza kuchukuliwa
hatua kubwa zaidi.
“Kanuni hazituruhusu kuzungumzia michezo niliyokwishaiamua huko
nyuma, lakini nikwambie ule mchezo niliuchezesha kwa sheria, kanuni, taratibu
na busara kama mwamuzi mwenye beji ya Fifa kwa kuwa ni mchezo mkubwa.
“Kama mtu ataona sikuwa sahihi au niliwakandamiza basi wanaweza
kukusanya ushahidi na kufuata ngazi za kunishitaki kwenye vyombo husika vya juu
hata Fifa,” alisema Nkongo.
Uongozi wa Simba pia umekuwa ukilalamika kuhusiana na kadi ya
njano ya mapema ya beki wake, Juuko Murshid, kuhusiana na hilo bila kutaja
jina, Nkongo anafafanua: “Mimi ni mwamuzi ‘senior’, mafunzo yangu yananiruhusu
kuwasoma wachezaji ndani ya dakika 15 za mwanzo na kutambua nani anataka
kuharibu mchezo, huyo nitakayembaini Fifa wanasema: ‘Destroy him, before he
destroy your game’ na ndicho kilichotokea.”
0 COMMENTS:
Post a Comment