Na
Saleh Ally
SAA
24 baada ya beki Juma Said Nyosso kumtendea udhalilishaji nahodha wa Azam FC,
John Bocco huku uongozi wa Mbeya City ukiwa kimya, nikapata hofu kubwa kutokana
na uwezo wao wa uendeshaji wa mambo yao.
Sikuusikia
tena uongozi wao kupitia kwa yule msemaji wao mchanga, Dismas Ten akisema
lolote. Walibaki kimya ikiwa ni dalili tosha ya kuonyesha kwamba hawakukerwa na
jambo lile.
Jumatano
Januari 28, mwaka huu, Nyosso alifanya kitendo kama hicho kwa mshambuliaji wa
Simba wakati huo, Elius Maguli ambaye hakika alikuwa muungwana hata kwa vyombo
vya habari, alitoa ushirikiano wa juu kabisa kwa Blog hii na gazeti la
CHAMPIONI licha ya kwamba alidhalilishwa.
Wako
waliodai Championi limemdhalilisha Maguli, matusi, maneno makali yalielekezwa
kwangu na timu nzima ya Championi. Mpango ukapangwa huko Mbeya na kabla
tukaunasa kwamba zinafanyika kampeni gazeti hili lisinunuliwe na mashabiki wa
Mbeya City.
Tuling’amua
baadhi ya viongozi wa klabu hiyo walioshirikiana na baadhi ya viongozi wa
matawi katika hilo. Siku moja kabla ya mechi ya Mbeya City dhidi ya Yanga kwenye
Uwanja wa Sokoine, tuliandika kuhusiana na mpango huo na siku iliyofuata
walitundika uwanjani bango likiwa na rangi za klabu hiyo, kwamba mashabiki
wasisome gazeti la Championi.
Ajabu
sana, uongozi wa Mbeya City haukuwahi kusema lolote kuhusu hilo kuonyesha kiasi
gani wanajua mpango mzima.
Lakini kamwe hatukuwa na kosa, badala yake Nyosso
aliyefanya ujinga ndiye walipaswa kumuonya. Hivyo ilionyesha pia baadhi ya
mashabiki wa Mbeya City wakiongozwa na viongozi wachache kutokana na uchanga
wao katika masuala ya soka, walishindwa kujua walichokuwa wanakitetea kwamba
kinawapaka matope.
Walitaka
Nyosso aendelee au alichofanya kifichwe? Kumbe hawakuona kwamba ni aibu kwa
timu ambayo ni changa sana na inahitaji nidhamu ya juu kabisa kufikia hapo.
Mwandishi
wetu, Sweetbert Lukonge alikuwa katika wakati mgumu akataka kupigwa na
mashabiki wa Mbeya City ambao walipangwa. Lakini mashabiki wa Yanga waliosafiri
kutoka Dar es Salaam wakamuokoa, tunawashukuru kwa hilo.
Ukweli,
kawaida unaonekana mbaya. Lakini kama kawaida yetu kama timu ya kikosi cha
Championi, mambo yakaendelea na tunaendelea kuongoza kwa kuweka mambo wazi hasa
maovu hadi hapo wachezaji wote watakaponyooka.
Safari
hii, Nyosso amerudia kitendo kama hicho, kwa kuwa Championi hatukuwa waoga
mwanzoni, wengine nao wameingia ujasiri wameripoti tukio hilo baya kabisa
kufanyika tena likifanywa na mtu mmoja ndani ya miezi minane.
Mbeya
City wamekaa kimya kama ilivyokuwa mwanzo, huenda wanajipanga kumtetea Nyosso
ambaye wao wanaamini ni jasiri, anapigania timu yao na huenda akawa shujaa.
Mbeya
City wamekaa kimya bila kujua wanaharibu uhusiano wao na wadhamini kama Bin
Slum Tyres, wanaowadhamini kupitia betri bora za RB, Coca Cola na wengine
wanaoshirikiana nao kupitia TFF kama Vodacom na Azam TV.
Swali
kwa wale mashabiki wachache wa Mbeya City wasiojielewa, wako tayari kuweka
bango jingine kuwa Championi na vyombo vingine vya habari visisomwe Mbeya?
Kama
sivyo, wako tayari kuungana na timu ya Championi kukanyaga na kuangamiza upuuzi
kama huo wa Nyosso ambao ni adui mkubwa wa soka?
Nyosso
hapaswi kusamehewa, aliomba msamaha. Nasi tukamsaidia kusambaza kwamba anaomba
Maguli amsamehe na kamwe hatorudia tena kitendo hicho ambacho aliona ni aibu
kubwa hata kwake na familia yake.
Lakini
leo amerudia, ajabu dhambi ile dhidi ya Maguli aliitenda kwa mkono wa kushoto.
Safari hii amefanya vilevile kwa Bocco kwa mkono wa kulia. Ingekuwa
tunazungumzia mshambuliaji, tungesema “anapiga miguu yote”. Hivyo ni mzoefu,
hatari kwelikweli na hataacha maana amezoea.
Tayari
sasa Amir Maftah amejitokeza na kusema Nyosso alimfanyia yeye akiwa Yanga
wakicheza dhidi ya Simba, akakasirika na kumpiga kichwa, akatolewa nje kwa kadi
nyekundu na watu wakasema ‘aliitafuta’ kwa kuwa alihongwa na Simba.
Achana
na hivyo, kuna shutuma nyingine dhidi ya Joseph Kaniki kwamba alifanya hivyo
Morogoro, akiwa Simba, akapigwa ngumi na Kaniki aliyetolewa kwa kadi nyekundu.
Kama
tuhuma hizi, zote ni kweli, kweli huyu mtu atajirekebisha?
Nafikiri
kabla ya TFF, Mbeya City lazima wasimame na kuzungumza jambo ikiwezekana
kuwaomba radhi mashabiki wao wengi ambao ni waelewa pamoja na wadhamini wao kwa
kuwa wote sasa wamechafuliwa na upuuzi wa mpuuzi mmoja tu. Jamaa feki kweli.
Mimi wasiwasi wangu Nyoso ni miongoni mwa wale wanaotaka sheria ya ndoa moja itumike,maaana haiwezekani kila siku kuwatomasa wenzake maungo mateke!
ReplyDeleteJamani tusimvumilie huyu jamaa hasiwe katumwa na mataifa ya magharib kuuneza utamaduni ambao hata rais Mugabe jana ameukemea pale UN.