Na Saleh Ally
KAMA unakumbuka
ilikuwa muda wa saa 11 kasoro hivi wakati nahodha wa Mbeya City, Juma Nyosso
alipotenda kosa la kumshika makalio nahodha wa Azam FC, John Bocco.
Nyosso alifanya
hivyo kwa makusudi, kitendo hicho cha wazi cha udhalilishaji kwa Bocco ambaye
kamwe hakuwahi hata kuingia kwenye kashfa ya ugomvi.
Bocco ni
mchezaji anayejituma sana, mchezaji ambaye ameonyesha mifano mingi likiwemo
kuwaonyesha vijana kwamba si lazima Yanga au Simba pekee, ndiyo unaweza kupata
mafanikio.
Amewahi kuwa mfungaji
bora akiwa Azam FC, amewahi kuipa ubingwa Azam FC na yuko kwenye timu ya taifa
akitokea Azam FC.
Bocco anaweza
kuwa mwalimu mzuri kwa vijana wengi wanaochipukia kuupenda mchezo wa soka hapa
nchini.
Amekutana na dhahama hiyo kutoka kwa Nyosso ambaye ni mwalimu mbaya na wa hovyo kabisa. Tena mwalimu asiyefaa, mtu mchafu na asiye na mapenzi na wengine.
Kwani wakati
Nyosso anamfanyia hivyo Bocco, tayari alikuwa amefanya kitendo kama hicho hapo
kabla, miezi kadhaa iliyopita wakati Mbeya City ilipocheza na Simba, msimu
uliopita.
Alifanya
hayohayo kwa Elius Maguli wa Simba wakati huo. Jambo ambalo liliwashangaza
wengi, ingawa likashangaza zaidi kwa wadau kuvishambulia vyombo vya habari
vilivyoonyesha uchafu huo.
Wengi walitaka
alichofanya Nyosso, kufichwa. Uongozi wa Mbeya City haukuwa na tofauti kubwa na
wahusika, yaani walioona Nyosso hakukosea.
Kwani
hawakuwahi kusema alichosema ni kitu kibaya wala kumpa onyo. Lakini hawakuwahi
kumuomba radhi Maguli na Simba au kuwaomba radhi mashabiki wao.
Nyosso
akafungiwa mechi nane, badala ya kuuona ubaya wake, baadhi ya mashabiki wa
Mbeya City, wakiungana na baadhi ya viongozi wageni kwenye mpira wakaungana
kuitetea ‘haki’ ya Nyosso.
Nyosso pekee
ndiye aliomba msamaha kwa Maguli na kusema anajutia jambo hilo. Akasisitiza
hatorudia, akasisitiza amejisikia vibaya, akaongeza wapenda soka nchini
wasimtenge.
Safari hii
karudia kwa mara nyingine, hadharani vilevile na kila mmoja ameuliza swali
hili. “Nyosso, amerudia tena?”
Kwa nini
wanasema hivyo, kwa kuwa vyombo vya habari hasa blogu hii na gazeti la
CHAMPIONI vilianika hilo waziwazi tofauti na wengi waliotaka lifichwe.
Sasa swali,
uongozi wa Mbeya City haujaliona hili. Kukaa kwake kimya kwa zaidi ya saa 24
maana yake nini? Hawajali au haliwahusu!
Katika tukio la
kwanza, hawakuomba ladhi kwa mashabiki, wapenda soka wala wadhamini wao ambao
wakati tukio la Nyosso linatokea alikuwa amevaa nembo za kibishara za kampuni
au bidhaa zao.
Lengo la
wadhamini ni kukuza biashara zao. Si kujidhalilisha na kuishusha biashara. Je,
Mbeya City hawalioni hilo au wanasubiri hadi wakumbushwe kama hivi, au
walaumiwe, au iweje?
Kama wamekuwa
watetezi kwa Nyosso, basi wawe watetezi katika heshima ya Mbeya City ambayo
haipaswi kuangushwa na Nyosso pekee wakati imejengwa na kupiganiwa na wengi
sana.
Najua Mbeya
City ni changa, kweli ina viongozi wachanga sana katika mchezo wa soka. Huu
ndiyo msimu wao wa pili Ligi Kuu Bara, kisoka kuwaita ndiyo wanachipukia si
vibaya sana.
Lakini bado
wana nafasi ya kujifunza haraka na kuweza kusoma alama za nyakati kwamba
kipindi ni kipi na kipi wanatakiwa wafanye haraka.
0 COMMENTS:
Post a Comment