KAVUMBAGU |
Na Saleh Ally
SIMBA imecheza mechi nane, imeshinda
sita na kupoteza mbili. Ina pointi 18 katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa
Ligi Kuu Bara.
Hauwezi kusema Simba ina mwendo mbaya
sana, lakini kwa rekodi za misimu mitatu iliyopita zinaibana kwa kuwa mashabiki
na wanachama wake wanataka kuiona ile Simba isiyofungika kirahisi, yenye
heshima ya kumtandika kila aliye mbele yake.
Mashabiki na wanachama hao wanataka
kuiona Simba ambayo ikishindwa kuwa bingwa basi itamaliza katika nafasi ya
pili. Je, kikosi cha sasa katika mwonekano wa mechi hizo nane kinaweza kufanya
hayo?
Katika hali ya kawaida, jibu sahihi ni
hapana. Kikosi cha Simba hakijafikia hapo kwa kuwa kinaonekana ni tegemezi
katika sehemu mbili muhimu jambo ambalo ni hatari sana.
Mfano nianzie upande wa Yanga. Kama
utasema Donald Ngoma ni hatari sana, akikosa basi ujue Amisi Tambwe atakuumiza,
akikosa yeye kuna Malimi Busungu au Simon Msuva ambao nao si rahisi kukukosa.
Kwa upande wa Simba inaonekana
mshambuliaji Hamis Kiiza akishindwa kufunga, Simba ipo matatani pia ni nadra
mwingine kuibuka na kulibeba jahazi katika wakati mgumu labda bao la ‘fruku’.
Ingawa mwanzo Simba walikuwa wagumu
kuhusiana na hilo, sasa wanaanza kuiona halisi na wanakubali kwamba hawana safu
bora ya ushambuliaji ndiyo maana wameanza mipango kuhakikisha wanafanya
mabadiliko wakati wa dirisha dogo.
Moja ya wachezaji ambao walikuwa sahihi
kwao kwa kipindi hiki ni Didier Kavumbagu ambaye amekuwa akibaki katika benchi
katika kikosi cha Azam FC kwa kuwa anaonekana si chaguo la kwanza kwa Kocha
Stewart Hall raia wa Uingereza.
Hall amekuwa akimtumia Kavumbagu kwa
nadra, Simba wameona angewasaidia ambalo ni jambo sahihi kabisa kwa kuwa haina
mshambuliaji bora na hata wale wawili wa kigeni, Simon Sserunkuma kutoka Uganda
na Pape N’daw wanaonekana ni ‘mizigo’ tu.
Wakati Simba inamtaka Kavumbagu, Hall
ameendelea kutia ngumu, hajakubali hata kumpeleka kwa mkopo Simba kwa kuwa
anajua akienda itakuwa ni yeye kujiongezea ugumu.
Ukiachana na Kavumbagu, Hall ana kitita
cha washambuliaji ukianza na Allan Wanga (Kenya), Kipre Tchetche (Ivory Coast)
na Ame Ali na John Bocco wote raia wa Tanzania.
Bado ana wachezaji kama Farid Mussa na
Ramadhani Singano anaoweza kuwatumia kama washambuliaji wa pili, yaani namba
10.
Lakini bado hataki Kavumbagu aondoke.
Yeye Kavumbagu anajua hatari ya kukaa benchi, anahitaji kucheza timu ya taifa
ya Burundi ambayo ili achaguliwe lazima awe na nafasi ya kwanza katika kikosi
cha kwanza.
Hall anakuwa mjanja zaidi, haangalii
matakwa ya Simba na Kavumbagu. Anaangalia yeye anataka nini, kikubwa kwake ni
kuepusha kuipa Simba silaha zaidi ili iwe imara.
Kuyumba kwa Simba na kushindwa kuwa na
safu kali ya ushambuliaji ni sawa na ule msemo wa ‘Adui mwombee njaa’.
Anajua mpinzani wake mkubwa kwa kipindi
ni Yanga ambayo ina washambuliaji wengi na ina nafasi kubwa ya kutetea taji
lake. Hivyo kuwapa Simba mshambuliaji ambaye anaamini ni bora ni sawa na
kuwaamsha ili wazidishe tena upinzani ambao mwisho utakuwa unamuumiza Hall na
kikosi chake.
Simba imefunga mabao tisa katika mechi
nane. Azam FC imefunga mabao 15 katika mechi hizo na Yanga ni kinara kwa kuwa na
mabao 20.
Utaona hapa, upinzani mkubwa ni kwa
Yanga. Hivyo ana haki ya kumzuia Kavumbagu ambaye ikiwezekana mara kadhaa
atakuwa ‘akimlambisha ice cream’ kwa kumpa nafasi ya kucheza mechi mojamoja.
Kuendelea kumbakiza Kavumbagu Azam, pia
ni kuwanyima silaha Simba ambao watalazimika kuhaha kupata mshambuliaji
mwingine. Hauwezi kujua, wanaweza kufeli tena kama ilivyokuwa kwa N’daw na
Sserunkuma ambao sasa hakuna ubishi tena wanatakiwa kuondoka.
Kuendelea kumzuia Kavumbagu ndani ya
Azam, kwa Hall kunaweza pia kukawa na faida kwa kuwa katika suala la
washambuliaji kama walivyo wachezaji wengine, hauwezi kujua maana kuna suala la
majeruhi au mchezaji mpira tu kumkataa.
Mfano, Mambo yamekuwa magumu kwa Wanga
au Bocco, basi Kavumbagu anaweza kupewa nafasi ya kuinua jahazi kama ilivyokuwa
juzi wakati alipoichezea Azam dhidi ya JKT na kufunga bao lililoisadia kushinda
kwa mabao 4-2 na kupaa hadi kileleni.
HALL AKIWA NA PLUIJM WA YANGA |
Kwa hili la Kavumbagu, Hall anaonyesha
ni kocha mwenye mipango anayeweza kujua anachokifanya kwa maana ya kuangalia
mbele.
Juzi alitoa kauli moja baada ya Azam
kuitwanga JKT. Kwamba wanachotafuta wao si kukaa kileleni kwa maana ya nafasi,
wanachokipigania ni pointi tatu ikiwezekana katika kila mechi.
Hapa utaona
ujanja wa kocha huyo ambaye anajua wanachotaka hasa ni kipi akijua kupatikana
kwa pointi, ndiyo kutakapowapa nafasi bora na ya uhakika na bila shaka ni moja
ambayo ndiyo ubingwa.
0 COMMENTS:
Post a Comment