Totauti na timu nyingine za Ligi Kuu Bara
zilizotoa wachezaji katika timu za taifa, Yanga haijalala na imeanza na mazoezi
licha ya kubakiwa na wachezaji wachache kikosini.
Juzi Alhamisi kwenye Uwanja wa Chuo cha
Polisi Kurasini, Dar es Salaam, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm alikuwa
makini kuwafundisha wachezaji sita tu kwani wengine hawakufika mazoezini hapo
huku wengi wao wakiwa timu za taifa.
Wakati Yanga inayoshika nafasi ya pili
katika ligi, ikianza harakati zake za kujiandaa na mechi za ligi kuu
zitakazochezwa mwezi ujao, Simba ya nne, yenyewe imepumzisha wachezaji wake
hadi Novemba 17 watakapoanza mazoezi na vinara Azam FC yenyewe itaanza mazoezi
Desemba 6 au 7, mwaka huu.
Walioudhuria mazoezi ya Yanga, juzi ni
Thaban Kamusoko, Geoffrey Mwashiuya, Pato Ngonyani, Benedict Tinoko, Oscar
Joshua na Deogratius Munishi ‘Dida’ na jana akaongezeka Deus Kaseke.
Hata hivyo, katika mazoezi hayo Pluijm
aliwekea msisitizo zoezi la kupiga mashuti na namna ya kukabana ambapo kutokana
na uchache wa wachezaji waliongezwa chipukizi wa kikosi cha vijana.
Wachezaji wa Yanga waliopo Taifa Stars
ni Ali Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Nadir
Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela, Simon Msuva na Malimi Busungu.
Waliopo timu ya taifa ya Zanzibar,
Zanzibar Heroes inayojiandaa na Kombe la Chalenji ni Juma Makapu na Simon
Matheo. Rwanda ameenda Amissi Tambwe wakati Togo ilimchukua Vincent Bossou.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment