BENTALEB (KUSHOTO) AKIICHEZEA SPURS AKIMILIKI MPIRA MBELE YA ALEX SONG WA WEST HAM UNITED NA CAMEROON. |
Kiungo wa Tottenham Hotspur na Algeria,
Nabil Bentaleb amesema licha ya kutoijua vyema Taifa Stars na soka la Tanzania,
ana uhakika timu yake itapata ushindi katika mchezo wa leo wa kufuzu Kombe la
Dunia 2018.
Bentaleb mzaliwa wa Lille, Ufaransa,
alisema ana matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi mzuri katika mchezo huo
utakaochezwa kuanzia saa 10:00 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kutokana
na uzoefu walionao.
Akizungumza na Championi Jumamosi,
Bentaleb ambaye alikuwemo katika kikosi cha Spurs kilichotoka sare ya bao 1-1
na Arsenal, wikiendi iliyopita kwenye Ligi Kuu England, alisema: “Ushindi wetu
hautokuwa rahisi kwani wengi wetu hatuijui Tanzania vizuri.
“Mimi ndiyo mara yangu ya kwanza kuja
Tanzania na sijui lolote kuhusu wachezaji wala soka la hapa, lakini lengo letu
kuu ni kupata ushindi na hicho ndicho kilicho kichwani mwangu.
“Tunajua wenyeji wamejipanga ili
wasifungwe nyumbani lakini tambua kuwa hii ni mechi ya kufuzu Kombe la Dunia na
kila mtu anataka kuandika historia ya kucheza michuano hiyo mikubwa, hivyo kazi
itakuwepo.”
Nyota huyo ambaye anaichezea Spurs
tangu mwaka 2013, ameichezea Algeria mechi 17 na kufunga mabao matatu tangu
alipoitwa kikosini kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
0 COMMENTS:
Post a Comment