Kocha
mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Abdallah Kibadeni
ametangaza kikosi cha wachezaji 21 kujiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji
itakayoanza kutimua vumbi Jumamosi Novemba 21, nchini Ethiopia.
Kibadeni
anayesaidiwa na kocha msaidizi Juma Mgunda, amesema wachezaji aliowaita wapo
katika hali nzuri na wamekua wakifanya mazoezi na kikosi cha Taifa Stars ambapo
wao kama benchi la ufundi wamepata nafasi ya kuwa nao kwa muda mrefu na
kutambua maendeleo yao.
“Tumechagua
wachezaji kulingana na mahitaji ya timu, tumekua na wachezaji hawa kwa muda
mrefu katika vipindi mbalimbali, tuna amini tuliowachagua watafanya vizuri
katika michuano hiyo mikongwe barani Afrika” amesema Kibadeni.
Wachezaji
walioitwa ni magolikipa, Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam), Said
Mohamed (Mtibwa Sugar), walinzi Shomari Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Simba),
Mohamed Hussein (Simba), Hassan Isihaka (Simba), Salim Mbonde (Mtibwa), Juma
Abdul (Yanga) na Kelvin Yondani (Yanga).
Viungo
Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Said Ndemla (Simba), Salum Telela
(Yanga), Salum Abubakar (Azam), Deus Kaseke (Yanga), washambuliaji John Bocco
(Azam), Elias Maguri (Stand United), Ibrahim Hajibu (Simba), Malimi Busungu
(Yanga) na Saimon Msuva (Yanga).
Michuano
ya Kombe la Chalenji inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 21 na kumalizika
Desemba 6, ambapo Kilimanjaro Stars imepangwa kundi A, lenye wenyeji Ethiopia,
Rwanda na Somalia.
0 COMMENTS:
Post a Comment