Na Saleh Ally
Kiungo Thabani Kamusoko ameweka rekodi mpya ya kufunga bao katika sekunde za mwisho kabisa za mchezo baada ya kufunga bao pekee wakati Yanga ilipoimaliza African Sports 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, juzi.
Kamusoko, raia wa Zimbabwe, alifunga bao hilo katika dakika tano za nyongeza ikiwa ni dakika ya 4 na sekunde 28, zikiwa zimebaki sekunde 32 tu mwamuzi apulize kipenga kumaliza mchezo.
Mechi ilionekana kama imeisha na krosi ya Haji Mwinyi ilipanguliwa na kipa wa African Sports na kuzua kizaazaa kabla ya bao hilo kupatikana na kuirejesha Yanga kileleni mwa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 27.
Bao hilo la shuti baada ya Kamusoko kupokea pasi ya kichwa ya Mzimbabwe mwenzake, Donald Ngoma, limefanya kuandikwa kwa rekodi kuwa bao lililofungwa sekunde za mwisho kabisa za mchezo ndani ya kipindi cha misimu mitano kuanzia msimu wa 2011-12.
Wengine waliofunga mabao katika dakika za 90 kwa msimu uliopita na huu lakini haikuwa katika sekunde za mwisho kabisa kama bao la Kamusoko ni Emmanuel Okwi (Simba ilipoilaza Mtibwa Sugar bao 1-0 ilikuwa Machi 14, 2015) na Nassoro Kapama Ndanda ilipoitwanga Kagera Sugar 2-1 (ilikuwa Januari 25, 2015).
Wengine waliopachika mabao ya dakika 90 ni pamoja na Amissi Tambwe, Rashid Mandawa, John Bocco na Donaldo Ngoma aliyefunga Yanga ilipoitwanga Mtibwa Sugar kwa mabao 2-0, hiyo ilikuwa Septemba 30, 2015.
Fully Maganga, Kipre Tcheche pia ni kati ya washambuliaji wanaoingia katika rekodi hiyo ya wale waliofunga mabao katika dakika ya 90 ya mechi pia kinda Rafael Alpha wa Mbeya City ambaye alifunga penalti katika mechi mbili tofauti katika muda huo.
0 COMMENTS:
Post a Comment