December 23, 2015


Na Saleh Ally
UNAKUMBUKA Manchester United iliyokuwa inaongozwa na Roy Keane au ile Arsenal chini ya Patrick Vieira? Kila mmoja alikuwa anafanya kazi yake kweli.

Kama huko ni mbali sana kwako, nakukumbusha Rio Ferdinand alipokuwa nahodha wa Manchester United. Namna alivyokuwa akiwaongoza wenzake na kwa kiasi kikubwa alikuwa akifanya kazi ya Kocha Sir. Alex Ferguson.

Nahodha huwa kiungo, anawaunganisha wenzake pia anakuwa mwakilishi wa kocha uwanjani. Nahodha anakuwa ndani ya uwanja, anaweza kuwafikia na kufikisha mambo mengi haraka.

Kwa upande wa Simba, nitakukumbusha mtu mmoja anaitwa Juma Kaseja. Kipa huyu aliondoka Msimbazi kwa figisu, hakupewa heshima yake, lakini kazi yake haiwezi kusahaulika.

Unakumbuka kipindi kile, mpira unaposimama tu, utaona anawaita wenzake na kuanza kuzungumza nao mambo kadhaa ambayo anakuwa ameyaona.

 Mfumo wa utazamaji makosa katika timu uko hivi; namba tisa na namba tano au kila mmoja anapewa nafasi kubwa ya kusoma kinachotokea kwa kuwa mnaposhambulia mabeki wanakuwa wanatazama na mnaposhambuliwa mara nyingi namba tisa anakuwa juu na kupata nafasi ya kuona zaidi.

 Kipa ndiyo anakuwa na nafasi kubwa zaidi. Lakini hilo halitoshi, kiongozi bila kujali ni nafasi ipi, anatakiwa kuwa ni mtu mwenye sauti inayosikika na kueleweka kwa wengine. Anaweza kuzuia hata kitu kisifanyike au mwenzake mwenye jazba anaweza kupungumza hizo jazba baada ya kusikia sauti yake.

 Simba imekuwa ikiendelea kuyumba kwa misimu mitatu sasa huu ni wa nne. Kati ya tatizo linaloisumbua timu hiyo licha ya kuwa na makocha tofauti ni uongozi wa ndani ya uwanja.

 Simba haina mtu kama Kaseja kwa maana ya kiongozi wa uwanjani lakini Simba haina nahodha imara ambaye anaweza kuwasimamisha wenzake dakika moja au nusu dakika akiwafafanulia jambo na wakamsikiliza na kumuelewa.

ISIHAKA

Nahodha wa sasa wa Simba ni Hassan Isihaka, kijana ambaye huu ndiyo msimu wake wa pili wa Ligi Kuu Bara. Kamwe hauwezi kumuita mchezaji imara badala yake unaweza kusema hivyo lakini lazima uongeze neno mtarajiwa.

 Simba imeamua kumpa unahodha Isihaka, lakini si mtu sahihi kulingana na kipindi hiki kigumu kwa timu hiyo. Huenda ni uoga au kuamini mambo kirahisi.

 Isihaka alipaswa kuwa mzoefu au tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa. Maana yake atakuwa ana vitu anavyopata vinavyoweza kuwasaidia wengine kupitia yeye.

 Mfano kuusoma mchezo, jiulize Isihaka anapokuwa amemuita Kiiza anataka kubadilisha kitu fulani. Au kumkemea kuacha uzembe akabe kwa nguvu.

 Katika kikosi cha timu ya taifa, Isihaka anajua kuwa atakaa benchi au jukwaani kabisa. Simba bado ni mchezaji anayekua, hivyo si sahihi kwa Simba sasa kumkuza hadi kumpa nafasi ya nahodha kama ambavyo imekuwa ikifanya kazi ya kukuza wachezaji kwa misimu mitatu na inakwenda wa nne sasa.

Kocha wa Simba, Dylan Kerr anapaswa kusaidiwa na kiongozi wa uwanjani ni mtu muhimu sana kwake. Kama Mussa Hassan Mgosi angekuwa ana nafasi ya kucheza basi lilikuwa ni jambo sahihi kabisa. Lakini ninaamini anajua kwamba kuna tatizo katika suala hilo la Isihaka lakini anaweza kuwa muoga kumbadilisha huenda kuna kitu fulani kitatokea.

 Ukiangalia mechi mbili zilizopita, Simba imetoka sare na zote ndiyo ilikuwa juu kabla ya wapinzani wake kusawazisha. Dhidi ya Azam FC, ilianza kufungwa bao la dakika ya kwanza tu, ikasawazisha na kuongeza lakini mwisho mechi ilikuwa mabao 2-2 baada ya Azam FC kusawazisha.

Mechi dhidi ya Toto Africans, Simba ilifungwa katika dakika ya 90, tayari za nyongeza zikiwa zimeanza kuhesabika tena baada ya Isihaka kuruka kizembe na kuruhusu mpira umfikie mfungaji.

Kumbuka enzi za Kaseja, unajua hapo ndiyo ungeona ukomavu wa nahodha au mwelekezi wa wenzake ambaye angekuwa akifanya mambo kadhaa ya kuhakikisha dakika mbili za mwisho Simba inamiliki mpira.

 Lakini utaona kila kipa Vincent Agbani akipata mpira alikuwa anabutua tu kwenda kwenye lango la Toto, sekunde chache mpira unarudi langoni mwake na mwisho wakafungwa bao hilo.

Lazima Simba waangalie mambo mengi sana, lakini lazima wakubali timu yao ni nzuri lakini si nzuri sana kufikia ‘level’ ya Simba. Mabadiliko yafanyike bila ya kujali kuna mtu atachukia na wakumbuke, misimu minne ya kuyumba na kuboronga, wanachosha.



0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic