December 11, 2015



 Na Saleh Ally
SIKU chache tu zimepita wakati TP Mazembe ikiwasili jijini Osaka nchini Japan, gumzo kubwa katika vyombo vya habari nchini humo alikuwa kipa Muteba Kidiaba na mshambuliaji hatari, Mbwana Samatta.

Kidiaba anakumbukwa Japan kwani takribani miaka minne aliiongoza TP Mazembe kucheza fainali ya michuano kama hiyo katika ardhi ya nchi hiyo dhidi ya Inter Milan.

Leo, TP Mazembe imetua Japan gumzo zaidi akiwa Mtanzania, Samatta ambaye ndiye amekuwa msaada mkubwa kuipa ubingwa wa Afrika.

Ndani ya kikosi hicho kuna Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu ambaye sasa ni kati ya wachezaji wanaoaminiwa au kutegemewa ndani ya kikosi cha Mazembe.

Hawa Watanzania wawili sasa wanaingia katika rekodi ya nchi yetu, wanakuwa Watanzania wa kwanza kucheza katika ngazi hiyo kubwa zaidi kimashindano kwa upande wa klabu. Wachezaji rundo wa Afrika, Ulaya na Amerika Kusini, pamoja na kuwa maarufu sana, bado hawajawahi kuipata nafasi hiyo.

Hata kwa wachezaji wa Afrika waliowahi kucheza ngazi hiyo, bado ni wa kuhesabika na ukizungumzia Afrika Mashariki, ndiyo hasa, utawapata kwa tochi.

Ulimwengu na Samatta, watakuwa huko na ndiyo maana nikaona uwe wakati mwafaka wa kukumbusha ili niwaguse ninaotaka kuwafikishia ujumbe wakati mambo yakiwa yanaendelea.

Nilisisitiza juzi, kwamba kupitia wawili hao wachezaji makinda au Watanzania wenye kutaka kutimiza ndoto zao wanaweza kujifunza. Pia itakuwa rahisi sana kujifunza kama anayeshuhudia kinachotokea atakubali, wawili hao hawakufika hapo kwa miujiza au uchawi, yaani ushirikina.


Kwani kama ingekuwa ushirikina ndiyo tegemeo lao, tunajua DR Congo kuna hadi shule za ushirikina, basi wasingefanikiwa hata kupata namba katika kikosi cha kwanza.

Sasa wao ndiyo tegemeo na moyo wa timu unapozungumzia suala la ushambulizi au kuifungia timu mabao.

Angalia TP Mazembe ilivyo sheheni wachezaji wenye vipaji au uwezo mkubwa kisoka, tena kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika, lakini bado Samatta ni tegemeo, Ulimwengu ana uhakika wa kucheza.

Hawa vijana, ukiwaangalia kwa haraka, ukawaona wakiendesha magari mazuri huenda unaweza kudhani mambo yalikuwa rahisi sana. Hakika wanastahili pongezi na shule kubwa inayomlazimisha yoyote mpenda maendeleo kukaa chini na kutafakari kwamba hakuna kinachopatikana kwa njia ya mkato.

Samatta na Ulimwengu hawakuwa na uwezo kifedha, hawakuwa hata na baiskeli. Kwanza walipigania kutimiza ndoto zao, hadi sasa inaonekana bado hawajafika lakini walipofikia, kila mmoja angetamani kufikia hapo.

Nani anatamani akiwa amelala ndani na ataweza kufanikiwa? Au nani anataka kufika hapo kwa kuamini mganga au sangoma anaweza kumfikisha hapo?


Hakuna asiyejua wachezaji kibao wanakwenda kwa waganga wa kienyeji ili kufanikiwa au kuwaumiza wenzao. Wanataka eti nyota zao zing’ae, jambo ambalo ni kichekesho mzembe kulazimisha kuwa na akili huku akiamini yeye ni bongo lala.
Kufanikiwa ni lazima kuwa malengo, mtu ajitume na kujitambua.

Samatta na Ulimwengu wanaondoa zile hisia Watanzania hawawezi kufika kokote. Leo walipo, wachezaji wa Afrika kwa asilimia 90 hawajawahi kufikia, wao wapo hapo halafu ni Watanzania.

Wangekuwa hapa nyumbani, kwa utaratibu mbovu uliojaa majungu, watu wasio na malengo na wanaoupenda mpira uwafaidishe wao kama ilivyo hapa nyumbani, basi wasingefika.
Hivyo hata ule ujasiri wao wa kuamua kuvuka na kwenda kucheza DR Congo, bado ni sehemu ya wengine kujifunza kwamba nje ya Yanga, Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar na wengine, yanaweza kupatikana mafanikio tena hata nje ya hapa nyumbani na pia si lazima iwe Ulaya.

Ushirikina, au kuamini uchawi huku ukiwa mzembe ni kujimaliza zaidi. Kama utasema wachawi sahihi basi ni Samatta na Ulimwengu na uchawi wao ni wa kitaalamu zaidi au hauhitaji malipo ili kuutumia.

SOURCE: CHAMPIONI


1 COMMENTS:

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic