![]() |
| NAPE |
Na
Saleh Ally
KIU
ya Watanzania wengi kulijua baraza la mawaziri la serikali ya awamu ya tano ya
Rais John Pombe Magufuli iliisha jana.
Serikali
ya Magufuli imekuwa ikifanya kazi ikiwa na viongozi wachache tu, lakini
imechachafya ile mbaya kwa kipindi cha mwezi mmoja na mabadiliko yameonekana.
Tumeona
namna vigogo kadhaa wa Mamlaka ya Mapato (TRA), bandari na kwingineko
walivyokumbwa na mafuriko ya Rais Magufuli na serikali bado haikuwa na baraza
la mawaziri.
Wakati
wa kampeni zake, Rais Magufuli aliahidi kuunda baraza dogo la mawaziri. Kweli
ametangaza mawaziri 30 tu, huku akiahidi kumalizia kuwatangaza wengine wanne
hapo baadaye.
Katika
baraza hilo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo ameteuliwa Nape
Nnauye kushika wadhifa huo na sasa wanamichezo watakuwa wamekata kiu yao ya
kujua nani atakuwa kiongozi au mwakilishi wao hasa serikalini.
Nape
amekuwa akikitumikia cheo cha Katibu Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM),
lakini sasa ni kwa ajili ya Watanzania wote na kikubwa ni kuendeleza
kinachotakiwa kupitia wizara yake.
CCM
ni kubwa, kuna mambo mengi yanayohusu vijana halikadhalika michezo na Nape
hatakuwa mgeni. Ndani yake kuna masuala ya wasanii ambao pia wamekuwa
wakihusishwa na mambo mbalimbali ya chama hicho kikubwa. Pia kwa kuwa waziri
huyo ni kijana kabisa, hakika kuna uwezekano wa kupatikana mabadiliko makubwa.
Wakati
Rais Magufuli alipoingia madarakani, alianza na staili ya kuvamia sehemu kadhaa
bila ya taarifa na kweli amekumbana na madudu kibao ambayo tayari yameanza
kushughulikiwa.
Katika
michezo kuna mambo mengi sana kama kweli ambayo yanahitaji mtu asiyetaka mchezo
ili kurudisha nidhamu na kuwafanya watu wa michezo sasa waamini nidhamu na
kujituma ndiyo kitu sahihi katika endelezaji wa mambo.
Inawezekana
katika michezo ukianzia soka, riadha, netiboli, ngumi za ridhaa na kulipwa
ndiyo kuna sehemu nyingi sana za kuvamia na kuleta mabadiliko.
Kama
Waziri Nape atapata sehemu ya kuvamia sehemu kibao atagundua kuna madudu mengi
kupindukia na watu wamekuwa wakiitumia michezo kuvimbisha matumbo na
kung’arisha nafsi zao.
Watu
wengi walio katika michezo kamwe hawaijali na kwa makusudi wala hawataki kupima
uwezo wao wa kiungozi badala yake wanatumia udhaifu wa wanamichezo wengi
kuwalaghai na hata kuwapa rushwa wawachague.
Kuna
ile methali isemayo hivi: “Akili haba na madaraka makubwa ni msiba”. Hakika
katika michezo tuna misiba lukuki, watu wengi hawajiwezi kiutendaji, lakini kwa
umahiri wao wa ushabiki, ushawishi mkubwa wa midomo au fedha zao unawapa nafasi
ya kuendelea kuwa viongozi wa juu lakini wasio na msaada wowote katika uletaji
maendeleo zaidi ya kutuachia msiba.
Ninajua
kabisa kuwa “vita vya bunduki haviamuliwi kwa fimbo”. Lakini namkumbusha Waziri
Nape kwamba “vya zamani si vya leo” na lazima akaze kamba ili watu waondokane
na yale mambo ya kuamini kila kitu kilikuwa kinakwenda kwa mazoea.
Watu
wamejimilikisha taasisi za umma au mali za Watanzania katika michezo na
wamejisahau kabisa kama ni za umma. Hawataki kukosolewa licha ya kwamba wana
uwezo mdogo na wanalijua hilo.
Kusiwe
na watu wanaotaka kusema wanaingiliwa kama wakikosolewa. Tafadhali pita kote
uone michezo inavyotumika kuwafaidisha wajanja wachache huku wanaoumia wakiwa
zaidi ya asilimia 90. Achana na ile ya Rais Magufuli ya kuvamia, katika michezo
hata ukitoa taarifa, kila utakapokwenda hakuna mwenye uwezo wa kuyafunika maovu
na uzembe wa makusudi unaofanyika kwa mikono yake. Lazima madudu hayo
yataonekana tu.








0 COMMENTS:
Post a Comment