Kombe la Ligi Kuu England lililopo
nchini kwa ziara maalum, jana Ijumaa mchana lilizuiwa kuingia katika viwanja
vya Mlimani City jijini Dar, kwa kile kilichoelezwa kuwa wahusika hawakuwa
wametoa taarifa.
Awali, kulikuwa na taarifa za kombe
hilo kufika Mlimani City saa 5:00 asubuhi lakini baadaye ikaelezwa lingefika
mahali hapo mchana saa 7:00.
Hata hivyo, mwandishi wa habari hii,
aliuliza kwa wahusika wa Mlimani City na kujibiwa kuwa hawana taarifa za ujio
wa kombe hilo. Kumbe wakati kombe likitakiwa kuwa Mlimani City saa 5:00,
wahusika walibadili ratiba na kulipeleka katika kituo kimoja cha redio na
runinga maeneo ya Mikocheni.
Hilo ni gundu juu ya gundu! Wakati
mabingwa watetezi wa Ligi Kuu England, Chelsea, hali ikiwa tete kwenye ligi kuu
msimu huu, nalo taji lao ambalo lipo nchini kwa maonyesho, limekumbana na mkosi
wa aina yake, baada ya zoezi hilo la kuonyeshwa kugonga mwamba Mliman City.
Hata hivyo, ilipofika saa 7:00 mchana,
msafara uliokuwa na kombe hilo uliwasili Mlimani City lakini ulizuiliwa na
walinzi mlangoni hadi saa 8:49 mchana
kwa kile kilichoelezwa kuwa hakukuwa na taarifa za ujio wake.
Mmoja wa walinzi wa Mlimani City
alisema hawakuwa na taarifa za ujio huo na hata uongozi wa mahali hapo nao
haukuwa na maelekezo yoyote, ndiyo maana walizuia msafara huo kwa sababu za
kiusalama.
Gari dogo la maofisa walioambatana na
kombe hilo, liliondoka Mlimani City na kuelekea mahali kwingine ambako
hakukufahamika, kwani hakuna mhusika aliyekuwa tayari kupokea simu kila
walipopigiwa. Pia hawakujibu hata ujumbe mfupi.
Kabla ya hapo ilionekana hakukuwa na mpangilio mzuri ambao ungewawezesha wadau wengi wa mchezo wa soka na mashabiki wa timu za Premier League wangeweza kuliona kombe hilo.
Hiyo ilitokana na mpangilio kuwa bomu na ulisababisha mashabiki wengi wa soka kuanza kulalamika kuhusiana na suala la hilo na wengine wakasusia kabisa.
0 COMMENTS:
Post a Comment