Aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya Geita Gold Sports, Selemani Matola, amefanikiwa kuanza vizuri kibarua chake katika timu hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 4-0 mbele ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Nyamkumbu Geita, juzi, Jumatatu.
Matola aliondoka Simba mwezi mmoja sasa kwa kile kilichodaiwa ni kutokuwa na maelewano mazuri na kocha mkuu wa timu hiyo Muingereza Dylan Kerr, na kutua kwenye timu hiyo inayoshika nafasi ya pili kundi C, ikiwa na pointi 15 nyuma ya vinara JKT Oljoro yenye pointi 17.
Matola amesema ameshukuru kwa kuiongoza kwa mara ya kwanza timu hiyo kwenye mchezo wa ligi na kupata ushindi, hivyo amewataka wachezaji wake na wapenzi wa timu hiyo kumpa sapoti ya kutosha ili aweze kuipandisha ligi kuu.
“Kutokana na kujiandaa vizuri tulikuwa na kila sababu ya kushinda, nimeongea na wachezaji wangu kuwa kila mechi tuifanye kuwa ni kama fainali hivyo tucheze kwa nguvu zote, nashukuru wameanza kunionyesha kuwa wamenielewa.
“Japo ligi ni ngumu lakini kama wachezaji wangu wataendelea kwa mwendo huu huu bila shaka tunaweza kabisa kupanda ligi kuu msimu ujao,” alisema Matola.
0 COMMENTS:
Post a Comment