Na Saleh Ally
Klabu ya Simba imefanikiwa kufanya mazungumzo na kumalizana na mshambuliaji Emmanuel Okwi ili arejee Simba kabla ya Desemba 15 ambayo ni Jumanne ijayo.
Lakini uongozi wa Klabu ya Sonderjyske umebadilika katika dakika za mwisho na kuongeza bei ya kumnunua tena, sasa Simba imeshindwa.
Awali makubaliano yalianza kati ya Simba na Sonderjyske iliyokubali kumuachia Okwi baada ya miezi sita tu kwa dau lilelile la Sh milioni 120.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amefunguka na kusema baada ya kumalizana na Sonderjyske, wakaanza mazungumzo na Okwi ambaye alikubali na wakawa tayari kulipa.
“Tukawa tayari kulipa fedha hizo lakini kwa awamu. Tukafikia mwafaka na mambo yakawa safi, lakini kabla hatujaanza jamaa wale wa Sonderjyske wakabadilika.
“Wamesema tena wanataka dola 440,000 (zaidi ya Sh milioni 928), jambo ambalo limekuwa gumu tena. Hata Okwi tumemueleza hali ilivyo ghafla, sasa sijajua nini kimewafanya wabadilike,” alisema Hans Poppe.
Gazeti hili liliandika kuhusiana na juhudi hizo za uongozi wa Simba kutaka kumrejesha Okwi, hali ambayo iliamsha matumaini kwa baadhi ya wanachama na mashabiki wa Msimbazi.
Hans Poppe amesema wanachama na mashabiki wa Simba, hawapaswi kuwa na hofu baada ya hilo kushindikana na kinachotakiwa sasa ni kuwaamini wachezaji walionao.
“Ninaamini tuna kikosi kizuri, (Paul) Kiongera, (Hamis) Kiiza, (Brian) Majwega, (Ibrahim) Ajibu na wengine wengi wataoongoza safu ya ushambuliaji na mambo yatakwenda vizuri,” alisema Hans Poppe.







0 COMMENTS:
Post a Comment