Kocha wa Makipa wa Yanga, Juma Pondamali, juzi Jumatano aligeuka kituko kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, baada ya kutaka kumtembezea kichapo Kocha Msaidizi wa African Sports, Mkenya, Razack Siwa.
Pondamali ambaye ni mmoja wa makocha wenye vituko, alimvaa Siwa mara baada ya mechi dhidi ya wapinzani wao hao katika Ligi Kuu Bara ambapo kisa kikitajwa kuwa ni Siwa kuomba kazi Yanga wakati anajua tayari Pondamali yupo klabuni hapo.
Memba wa benchi la ufundi la Yanga, walimzuia Pondamali kumshushia kipigo Siwa licha ya kuonekana kuwa na hasira na tayari alishaanza kurusha makonde hewani.
Alipoulizwa Siwa alisema: “Hivi karibuni nilipeleka barua ya kuomba kazi ya kuwa kocha wa makipa wa Yanga, kumbe kitendo hicho kimemkera sana Pondamali na hapa alikuja kutaka kunipiga kisa nimeomba kazi Yanga wakati najua yeye yupo.
“Sikutegemea kabisa kwa mtu kama yeye mwenye heshima kubwa hapa nchini kutaka kunipiga kwa sababu ya barua ya kazi, kusema kweli imenisikitisha sana,” alisema Siwa.
Upande wa Pondamali aligoma kuzungumza chochote juu ya tukio hilo kutokana na kukatazwa na baadhi ya viongozi wa Yanga waliokuwa wakimzuia kupigana.
Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, alionyesha kushangazwa na kitendo hicho, kwani baada ya kutulia kwa timbwili, alimfuata Siwa na kumtaka apuuze kilichotokea.
0 COMMENTS:
Post a Comment