Na Saleh Ally
KIUNGO Haruna Niyonzima, jana alijitokeza hadharani na kuomba radhi mbele ya mashabiki wa soka nchini.
Niyonzima raia wa Rwanda aliomba radhi kwa mashabiki wa soka lakini akianza na wale wa Yanga pamoja na wanachama wake, lakini pia viongozi wake.
Alieleza namna anavyojisikia, pia kusisitiza yeye ni binadamu. Nafikiri hiyo ni hali ya kiungwana kabisa ambayo inaonyesha wazi kwamba anajitambua na yuko tayari kutumikia adhabu ya makosa yake, ndiyo maana ameomba radhi.
Yanga kupitia katibu mkuu wake, Dk Jonas Tiboroha ilieleza uamuzi wake wa kuvunja mkataba na Niyonzima kutokana na suala la utovu wa nidhamu.
Wakati Niyonzima anajitokeza, taarifa za uhakika zinaeleza kwamba kiungo huyo mchezeshaji hakuwa amepewa barua ya kuvunjwa kwa mkataba na badala yake ndiye alikuwa akiidai.
Yanga walichukua uamuzi wa kuvunja mkataba mwisho kabisa baada ya kukutana na Niyonzima, mwisho wa kikao akatakiwa kuandika maelezo kwa maandishi lakini, lakini mwisho wake hakufanya hivyo kwa mujibu wa Yanga.
Kwangu ninaona kuna walakini mkubwa kwa kuwa Niyonzima anajulikana ni mtu wa aina gani. Kweli ana misimamo pale anapoona anaonewa, lakini si mtovu wa nidhamu na tumeona muda wote amekuwa Yanga amekuwa hazozani na viongozi.
Hivyo, Yanga wanaweza wakaiangalia kasoro hiyo ya kwanza kuhusiana na barua, kweli haijafika au kuna figisu zinafanywa ili mchezaji huyo aonekane hafai au kumgombanisha na wanachama tu!
Mimi binafsi, bado siamini kama Niyonzima baada ya kukaa kwenye kikao cha kamati ya utendaji, wakiwemo wajumbe wanaoheshimika kabisa pamoja na kocha wake, halafu kweli hakupeleka barua!
Yeye ameshasema alipeleka barua na anaamini ilipokelewa Jangwani. Hivyo, anapinga kabisa suala la kwamba hakupeleka hiyo barua ya utetezi, hivyo lifanyiwe kazi.
Pili ni suala la Yanga na uamuzi wa kuachana na Niyonzima, eti kwa kuchelewa mara mbili au tatu kurudi kambini, kwangu ni kichekesho cha aina yake kabisa. Hii ni kasoro nyingine ambayo ingekuwa jambo la busara kuliangalia kindakindaki na si kama linavyopitiwa sasa.
Nimeona kampeni moja ya kijinga kabisa, kutaka kuonyesha kiungo Thabani Kamusoko ni safi sana, hivyo Yanga haina shida na Niyonzima. Sijui nani huyo aliye nyuma ya kampeni hiyo chovu na inaungwa mkono na wengi wasiojua mpira.
Yanga inataka kuwa bora zaidi, hivyo inahitaji wachezaji bora kama Niyonzima na Kamusoko. Wote wawili wakiunganisha nguvu, Yanga inakuwa ni bora zaidi na ukizingatia sasa inaingia katika michuano ya kimataifa.
Achana na zile hisia, eti Niyonzima anakaa sana na mpira. Wewe unayesema ni kocha, au unajua kwa nini anakaa na mpira. Kwani hujawahi kuona Yanga inafanya vizuri chini ya Niyonzima. Mara ngapi anafanya vizuri akiwa na Rwanda ‘Amavubi’. Nani hajui ubora wa Niyonzima?
Ukituliza akili, utaona suala la Niyonzima lina kona nyingi. Inaonekana kuna ujanja unafanyika, inaonekana kabisa ndani yake kuna figisu ambazo zimelenga kumjaza makosa zaidi ya aliyonayo, mwisho aonekane hafai kabisa.
Kwa kuwa mimi si mfanyakazi wa Yanga, huenda nisijue kila kinachoendelea lakini ninaamini walio ndani watakuwa wanajua kuna tatizo, ndiyo maana nashauri kabla ya Yanga haijachukua uamuzi wa kumkabidhi Niyonzima barua mkononi, basi litakuwa jambo la busara kupitia tena suala hilo kwa umakini mkubwa na kupata uhakika ili kujiridhisha.
Iwapo Yanga watapata uhakika kwa asilimia mia, kweli Niyonzima ni tatizo, mtovu wa nidhamu. Basi bila shida, wanaweza kuchukua hatua walizozianza. Wakigundua kuna shida au figisu, hakika wala wasione shida kurudi nyuma na kumsamehe.
Yeye atajifunza, ila wao pia wanapaswa kuwa makini na kuangalia aliyehusika na jambo hilo au mtengeneza figisu kama ni mtumishi wa klabu, atupiwe virago kwa kuwa hatakuwa mtu sahihi kwa klabu hiyo unapozungumzia suala la umoja kwa ajili ya maendeleo.
0 COMMENTS:
Post a Comment