Ni kama utani lakini ukweli ni kwamba kocha wa heshima Bongo, Abdallah Kibadeni Mputa, amesema ni mara mia akutane na Simba kuliko maafande wa Mgambo JKT kwa kile alichosema Simba ya sasa inaishi kwa kucheza soka la kuwafurahisha mashabiki majukwaani.
Kauli ya Mputa imekuja baada ya timu yake ya JKT Ruvu kulala mabao 5-1 nyumbani mbele ya Mgambo juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Karume, Dar huku wakijiandaa kukipiga na Simba katika mchezo unaofuata keshokutwa Jumatano, Uwanja wa Taifa, Dar.
Akizungumzia mchezo ujao, kocha huyo ambaye Simba ni kama ‘mzazi’ wake, alisema anaijua nje-ndani Simba na falsafa zake zote na kutoboa siri kuwa huwa ni timu ya pasi nyingi zisizo za kusaka mabao, tofauti na Mgambo ambao juzi walilisakama lango la JKT mwanzo-mwisho na kuibuka na ushindi mkubwa.
“Kwa Simba ninayoijua, ni heri ukutane nao kuliko hawa Mgambo, unapokutana na timu inayocheza soka la pasi nyingi inakuwa ahueni kuwazuia kuliko Mgambo ambao wana soka la kasi, nguvu na mfumo wa ‘counter attack’ ndiyo maana mchezo ulituwea mgumu sana kwa leo (juzi),” alisema.
0 COMMENTS:
Post a Comment