Na Saleh Ally
KOCHA Mecky Maxime wa Mtibwa Sugar ni kijana wa Tanzania ambaye unaweza kusema anaijua na kuithamini kazi yake na huenda anapaswa kuwa mfano kwa wengine wengi sana, nitakuambia kwa nini.
Katika mechi tatu za Ligi Kuu Bara zilizopita ambazo Mtibwa Sugar ilicheza, kiwango chao cha uchezaji kimeonekana kuwa juu sana.
Hali kadhalika, mechi yao ya kwanza ya Kombe la Mapinduzi, wameonyesha uwezo mkubwa pia na kuipa Azam FC wakati mgumu kwelikweli, hakuna ubishi ilitoka kibahati sana kwa ile sare ya 1-1.
Katika Ligi Kuu Bara ambayo imesimama, Mtibwa Sugar iko katika nafasi ya nne ikiwa na pointi 27, wanaongoza Azam FC, wanafuatia Yanga halafu Simba. Nitakukumbusha tu, timu zote tatu juu ya Mtibwa zinafundishwa na makocha wa kigeni kutoka bara la Ulaya.
Stewart Hall wa Azam FC kutoka Uingereza, Hans van der Pluijm wa Yanga (Uholanzi) na Dylan Kerr wa Simba (Uingereza) halafu anafuatia Maxime, Made in Tanzania.
Ambacho najadili ni namna Mtibwa Sugar inavyoonyesha soka safi na kuzipa shida kubwa Yanga na Simba, pia Azam FC ambazo zina uwezo mkubwa kifedha. Zina gharama kubwa katika usajili na hata mishahara mikubwa ya wachezaji na makocha.
Usishangae, wachezaji watano au 10 wa Azam FC au Yanga, wanaweza kuwalipa mshahara wachezaji wote wa Mtibwa Sugar. Mshahara wa kocha wa Azam FC au Yanga, anaweza kumlipa Maxime na benchi lote la Mtibwa Sugar ambalo lina wachapa kazi wengine kama Zuberi Katwila na Patrick Mwangata.
Kama ni kujivunia Utanzania, basi benchi la Mtibwa Sugar, lenye vijana wote na wote wamecheza soka katika kiwango cha juu hapa nyumbani pia timu za taifa yaani Taifa Stars na Kilimanjaro Stars na leo wanafanya vema.
Mtibwa Sugar inapiga soka utafikiri Maxime na wenzake ndiyo makocha wa kigeni. Utafikiri Mtibwa Sugar wana mishahara mikubwa sana au wana wachezaji wengi kutoka nje ya Tanzania.
Lakini usisahau, kila mchezaji ambaye huonekana hawezi kucheza Yanga, Simba au Azam FC kwa Maxime atapata nafasi na kiwango chake kitarudi.
Angalia upande wa Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ au Hussein Javu ambao walionekana hawana lolote Simba na Yanga, sasa wanafanya vema sana.
Maxime ambaye wasiyemjua humuita Mexime anaonekana si mtu wa masihara linapofikia suala la kazi na amewafanya wengine kuwa hivyo na sasa wanapiga kazi kweli.
Utendaji kazi wa Maxime na wenzake, unatumbua jipu la utendaji wa kazi kwa Watanzania na makocha wa kigeni kwamba kuna tatizo kubwa sana.
Sitaki kusema timu kubwa zimekuwa zikitumia nguvu ya ‘ujanja’ kupata matokeo mazuri, lakini pia kunaonekana kujitambua kwa wanamichezo wengi Watanzania kuna tatizo, pia makocha wageni na wachezaji wazawa pia kuna tatizo.
Wachezaji wengi wanapopata mafanikio kidogo hasa ya kuongezewa mshahara, wanakuwa tatizo, wanashindwa kujituma na kuanza kuporomoka.
Vipi mchezaji wa Mtibwa Sugar anayelipwa chini mara tatu au nne ukilinganisha na mchezaji wa Azam FC au Yanga au Simba, awe na kiwango bora zaidi? Jibu ni kwamba wanapata muda wa kutosha wa mazoezi, akili na nguvu wanawekeza katika kazi yao.
Wachezaji wa Mtibwa Sugar wanaishi Turiani. Muda mwingi akili yao ni katika kazi yao ya soka. Wachezaji wengi wa Yanga, Simba wanataka kuchungwa utafikiri wanyama. Si sahihi mtu achungwe ndiyo afanye kazi.
Lakini kiwango bora cha Mtibwa Sugar kwa kipindi hiki au kwa miaka miwili. Kinaonyesha makocha wazawa pia wanaweza kama wakipewa nafasi na kuaminiwa.
Wakati mwingine makocha hawana uhuru, mfano Kocha Kerr wa Simba, kila siku inayokucha anaangushiwa lawama tu na inaonekana kiongozi huyu hafurahii, mara yule hajaridhishwa. Kila kocha Simba sasa hafai kabisa!
Ndiyo maana nasisitiza, Maxime anaweza kuwa somo, lakini wachezaji wa Mtibwa Sugar ni somo pia kwa maana ya kazi nzuri wanayofanya. Hata Mtibwa Sugar ikipoteza mchezo, lakini utasema mpira umechezwa, labda hawakutumia nafasi tu.
Kingine cha mwisho, Mtibwa Sugar pia inaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuwa wako ‘siriaz’, pia wana uwanja wa mazoezi. Kocha anafanya mazoezi kulingana na alivyojipanga, tofauti na Yanga na Simba, wakongwe, wakubwa, lakini viwanja vya kudandia katika shule za msingi, sekondari na timu za veteran. Sijui watabadilika lini hawa!
1 COMMENTS:
ReplyDelete