February 19, 2016


MOSHA AKIWA OFISINI KWAKE SINZA JIJINI DAR ES SALAAM
Na Saleh Ally
WATANI wa jadi Yanga na Simba wanakutana katika mechi yao ya Ligi Kuu Bara, kesho na huenda ukawa ndiyo mwisho wa majigambo kwa kuwa jibu la nani mbabe litapatikana.

Mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ililala kwa mabao 2-0. Hapohapo zinakutana na aliyewahi kuwa mmoja wa viongozi katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis Mosha ni kati ya wanaofuatilia.

Mosha ambaye ni kati ya vijana matajiri wa Kitanzania, ana imani kubwa kwamba mechi hiyo itakuwa ngumu na mshindi atapatikana baada ya dakika 90.
Pamoja na hivyo, Mosha anaamini kuna mambo mengi yanayotakiwa kufanywa ili Yanga iweze kushinda mechi ya kesho.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Mosha anaelezea mambo kadhaa huku akisisitiza ndiyo msingi sahihi.

SALEHJEMBE: Kipi cha kwanza kinatakiwa kufanyika?
Mosha: Umoja na ukaribu wa makundi yote. Mfano wachezaji, mashabiki na uongozi kuwa pamoja kwa ajili ya timu na kusiwe na hisia za kutafutwa mchawi.

SALEHJEMBE:Mchawi kivipi Mosha?
Mosha: Unajua, kabla ya mechi hiyo ya watani kuna mambo mengi, suala la kutafuta mchawi kabla au baada ya mechi halina faida.


SALEHJEMBE:Unafikiri viongozi wawe karibu vipi, watoe ahadi au motisha ya kutosha?
Mosha: Kutoa fedha ni sehemu tu, lakini kuwapa wachezaji fedha pekee haitoshi. Viongozi wawe karibu nao, waonyeshe ni sehemu yao. Ikiwezekana waende kambini na kula nao hata kulala nao. Unakumbuka nikiwa mfadhili wa Ushirika Moshi, Simba ilikuwa inateseka sana, nilikuwa pamoja na wachezaji hadi kambini. Pia Moro United, waulize Simba watakuambia na nilipokaa Yanga kwa mwaka mmoja na nusu hivi, hawakuwahi kuifunga Yanga.

SALEHJEMBE:Unafikiri kweli viongozi wa sasa wanaweza kulala kambini kama enzi za akina Viran au Azim Dewji?
Mosha: Ninaamini inawezekana, kiongozi asijikwaze na kuona yeye si saizi ya wachezaji. Kwa kuwa ndiye kiongozi wao, basi awe nao pamoja.

SALEHJEMBE:Hauonekani tena uwanjani, uliondoka kabisa Yanga, kipi ulifeli?
Mosha: Sikufeli, ila niliona sisikilizwi. Nilitaka Yanga isiwe tegemezi kama sasa. Nilitaka Yanga isiyotegemea mtu mmoja, ikaonekana ni kama nakosea, nikaamua kuondoka.
Wanachama na mashabiki bado wanaamini kuifunga Simba na kuongoza ligi ndiyo kila kitu. Hilo si sahihi, baadaye yatakuwa ni mateso ya Yanga.
Ni timu kubwa lakini haina kitu, haina maendeleo. Leo Yanga na hata Simba wanatakiwa kujifunza kwa Azam FC? Kweli watu hawaoni, hawaumii na wanaona ushindi dhidi ya Simba pekee ndiyo unatosha!


SALEHJEMBE: Sasa tatizo ni lipi hadi inashindikana?
Mosha: Mfumo ni mbovu, Wanayanga pia hawaoni. Yanga inapaswa kuwa na vitega uchumi, kuna Mafia na Jangwani. Vikiendelezwa itajitegemea. Leo hakuna hata anayeuliza kwa kuwa kila mmoja anaona ubingwa na kuifunga Simba, inatosha kabisa! Si sahihi hata kidogo hasa ukizingatia Yanga imeanzishwa mwaka 1935, leo inajifunza kwa timu iliyoanzishwa miaka saba, nane iliyopita.

SALEHJEMBE:Lakini ulipaswa ubaki badala ya kuondoka!
Mosha: Niliona sieleweki, peke yangu nisingeweza. Nitabaki kuwa Yanga damu, lakini muda, fedha zangu ninaona nielekeze kwingine kwa kuwa nina biashara zangu.


SALEHJEMBE: Vipi utakwenda uwanjani Jumamosi?
Mosha: Hapana, nitaangalia tu mechi. Nilishakata tamaa, naona kila siku tuko palepale.

SALEHJEMBE: Uliwahi kusema kuhusiana na serikali kusaidia michezo, unaonaje kwa kipindi hiki?
Mosha: Bado kabisa, naendelea kushauri na kusisitiza, serikali ijitokeze na kusaidia kuweka mfumo bora katika michezo. Kila sehemu mambo ni ya kubahatisha, watu wako kwenye michezo kwa ajili ya siasa au maslahi yao pekee. Serikali inaona na haifanyi lolote.

Michezo ni furaha, afya na ajira. Hili linaihusu serikali, ikae kati na kusaidia ukuaji wa michezo kwa mfumo bora na sahihi.

KIKOSI CHA YANGA

SALEHJEMBE: Watu wanakuwa katika michezo kwa maslahi yao, fafanua kidogo…
Mosha: Mtu hajui michezo, kwa kuwa anajulikana, mwanasiasa au ana fedha. Basi anaingia kuongoza, mwisho wake ni matatizo tu. Nawashauri watu kuipa nguvu michezo. Wasaidie zaidi kuliko kujisaidia wao.

SALEHJEMBE: Nikimalizia, Yanga hata Simba, hufanya maandalizi makubwa katika mechi ya watani tu, wewe ulikuwa mmoja wao, huoni mnakosea sana?

Mosha: Hilo nakubali kuwa si sahihi, maandalizi bora yanatakiwa katika mechi zote. Mpira unaenda na historia, mechi hiyo inakuwa tofauti kutokana na historia ya timu zenyewe na klabu pia. Hivyo inafanya iwe hivyo, ingawa nashauri kuwa, maandalizi bora kwa kila mechi ni jambo bora zaidi.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic