Timu ya Simba juzi Jumamosi ilifanikiwa kupunguza pengo la pointi dhidi ya Yanga na Azam ambazo kwa sasa ndizo zinaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara zikiwa na pointi 39, lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.
Simba ilifanikiwa kupunguza pengo hilo kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya African Sports ya Tanga kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Jackson Mayanja, amesema kuwa endapo wachezaji wake watazingatia mambo matatu muhimu, wanaweza kuibuka mabingwa msimu huu. Mara ya mwisho Simba kutwaa ubingwa wa ligi ilikuwa ni 2012.
Mayanja alisema kama wachezaji wake wataongeza bidii mazoezini, wakazingatia kila kitu anachowaelekeza na kucheza kwa ushirikiano mkubwa bila kubaguana, basi ana uhakika wa ubingwa.
“Namshukuru Mungu kwa kila jambo, ikiwa ni pamoja na matokeo mazuri ambayo tunaendelea kuyapata katika mechi zetu tunazocheza, hakika ni jambo la kujivunia.
“Hata hivyo, wachezaji wangu kama wakizingatia mambo matatu ambayo binafsi nayaona kuwa ni muhimu sana, ambayo ni kujituma zaidi mazoezini, kuzingatia yote ninayowafundisha na kucheza kwa ushirikiano mkubwa bila ya ubaguzi hakika tunaweza kuibuka mabingwa ligi kuu,” alisema Mayanja ambaye amejiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea Coastal Union ya Tanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment