February 22, 2016


Na Saleh Ally
FURAHA waliyonayo mashabiki wa Yanga haina mfano. Wamemaliza kiu yao ya ubishi kati yao na mashabiki wapinzani wao, hawa ni wale wa Simba.
Klabu zote hizo zinatokea Kariakoo jijini Dar es Salaam, tofauti ya makazi yao ni kama kilomita moja hivi.

Lakini mashabiki wake wanatokea Tanzania nzima na nguvu ya klabu hizo ni kubwa kweli. Ndiyo maana wiki yote iliyopita ni majigambo, nani atamshinda nani.

Sasa ni Yanga, ndiyo watakuwa na nafasi ya kushangilia au kusherehekea kwa wiki moja zaidi baada ya kikosi chao kuituliza Simba kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, juzi ikiwa ni mara ya pili katika msimu wa 2015-16.

Sasa Simba hawawezi tena kupinga kwamba Yanga ni kiboko yao kwa msimu huu. Kama kuifunga, inaonekana waliisumbua sana kwenye Nani Mtani Jembe, mechi ambayo haipo tena. Huenda ni wakati wa Yanga kuendelea kuinyanyasa Simba.


Mchezo juzi:
Mechi ya juzi, ilitarajiwa kuwa nzuri, yenye mvuto sana. Lakini ikaenda tofauti kabisa hasa kwa upande wa Simba baada ya beki wake Abdi Banda kulambwa kadi mbili za njano ndani ya dakika tatu na baada ya hapo beki mwingine Hassan Kessy “akachoma nyumba”.

 Kimahesabu, Yanga ilifanikiwa kuimaliza mechi hiyo ndani ya dakika 17, tayari ikawa imepata matokeo na majibu yalikuwa wazi. Ushindi wa Simba ukashuka hadi 28% huku ikionekana nafasi ya kujikomboa ilikuwa sare tu.

Dakika ya 22:
Abdi Banda alilambwa kadi ya njano na mwamuzi Jonnesia Rukyaa baada ya kumvuta Donald Ngoma aliyekuwa akielekea katika lango lake.
Banda alikuwa anacheza nafasi ya beki wa kati, yaani namba nne na alionekana kuzidiwa kasi na Ngoma, akamvuta na kumwangusha, mwamuzi Jonnesia akatoa kadi ya njano, hii haikuwa na utata hata kidogo.


Dakika ya 25:
Ngoma tena anapata pasi ya pembeni nje ya 18. Wakati anaanza kuondoka, Banda anagundua itakuwa madhara, safari hii anamuwahi na kutanguliza mguu halafu anamsukuma kidogo kwa bega na kujaribu kuuwahi mpira, Ngoma kama ambavyo ingekuwa kwa mshambuliaji yoyote, anajirusha na mwamuzi anasema ni faulo.
Wakati mwamuzi anamsogelea Banda, hakuna aliyetarajia hata angetoa kadi. Nahodha wa mechi kwa upande wa Simba, Jonas Mkude, yeye alikuwa akilalamikia mwamuzi kwamba Ngoma anajirusha sana.

Ghafla anamuita Banda na kumpa kadi ya pili ya njano na kuunganisha nyekundu. Hakika haikuwa kadi sahihi hata kidogo, huenda wengi wakaona haya kusema kuhofia mambo ya kishabiki.

Hali halisi ya faulo ya pili, haimpi nafasi Jonnesia kutoa kadi. Banda hakumsukuma Ngoma kwa nyuma, wala hakumkata kwa nyuma au kuinua mguu na kumtega. Badala yake alimgonga kwa bega na “Football is game of Man”, kamwe watu hawawezi kucheza bila ya kusukumana. Ndiyo maana kuna faulo za kimpira, moja wapo ni hiyo ya Banda.

Hata kama Jonnesia anajua sana sheria 17, lakini faulo za kadi na bila kadi zinajulikana. Mwonekano wake ni dhahiri unapishana na hili si jambo geni kwa anayefuatilia soka.

Kadi hiyo ya Jonnesia, inaonekana kutoiadhiri sana Simba. Ingawa kwa maana ya plani, haraka kocha Jackson Mayanja alitakiwa kumtoa fowadi na kumuingiza beki.

Dakika tatu tu, tayari Banda alipata kadi mbili za njano na kuzaa nyekundu. Moja ikiwa ni kosa lake dhahiri (ile ya kwanza) na nyingine ni kosa la mwamuzi ambayo ni vigumu kuhakikisha alidhamiria kwa manufaa yake au ni kosa la kibinadamu.

Huenda kama ni kujifunza, Banda atajifunza kwa ile kadi ya kwanza, kwamba angeweza kuwa makini angeiepusha na kumnyima nafasi Jonnesia kutoa ya pili ambayo ni kosa lake mwamuzi la wazi. Hizi zilikuwa ni dakika tatu tu.

Kessy anamaliza:
Hata baada ya kadi, ingawa tahadhari iliongezeka kwa Simba, lakini iliendelea kucheza vizuri kabisa huku Jonas Mkude akitawala. Hakuwa na msaada mkubwa sana kutoka kwa Justice Majabvi ambaye huenda umri unaanza kumpa shida na tayari alikuwa amerudi nyuma kuonyesha kutokuwa na kasi sahihi.


Wakati inaonekana Simba kama wameizoea ile hali ya kuwa pungufu mtu mmoja na wangeweza kupambana, dakika ya 39, beki wa kulia, Hassan Kessy, anafanya kosa kubwa la kurudisha mpira mfupi, Ngoma anakimbia kasi na kuuwahi, anaudokoa unapita kushoto kwa kipa Vincent Agban, anazunguka na kuuwahi. Anaukwamisha wavuni kwa mbwembwe kabisa. Mchezo umeisha.

Simba yenye watu pungufu, ilitakiwa kwenda mapumziko ikiwa haijafungwa. Baada ya hapo ilikuwa ni kujipanga namna ya kuzicheza dakika 45 zilizobaki ikiwa ni pamoja na kumuingiza beki wa kati kwa kuwa Majabvi alikuwa haonekani na alipotea mara nyingi.

Dakika 22 kutoka kadi ya kwanza ya njano ya Banda hadi dakika 39 ni 17. Tayari Yanga wakawa wamemaliza mchezo. Kwani kutangulia kwa bao moja, presha kwa Simba ikawa ni 100% huku Yanga ikiwa sasa inachoangalia ni ushindi kwa zaidi ya 75%.

Ushindi kwa Simba, ilikuwa ni bahati nasibu tena. Ilichoangalia ni sare au kuepuka kufungwa mabao mengi. Ndiyo maana utaona Kocha Hans van der Pluijm wa Yanga, alimuingiza Simon Msuva mapema katika kipindi cha pili, akamuingiza Geofrey Mwashiuya. Yote hii ilikuwa ni kuiongezea Simba presha zaidi ili “iachie”.

Angetolewa Majabvi:
Kocha Mayanja alionekana kutulia na kutofanya mabadiliko baada ya kadi nyekundu ya Banda. Huenda aliona zimebaki dakika 5 ambazo angemaliza nazo hivyo na kufanya hivyo baada ya mapumziko.

 Kawaida, anapotolewa beki au mtu kupata kadi nyekundu, anayelengwa kutolewa anakuwa ni mshambuliaji. Hivyo haraka angeweza kutolewa Hamisi Kiiza au Ibrahim Ajib.


Lakini bado Mayanja alikuwa na nafasi ya kufanya kitu tofauti kama angetulia na Ajib na Kiiza wangebaki na huenda angeurekebisha mchezo.

Kabla ya kumuingiza beki Novatus Lufunga, angemtoa Majabvi ambaye alionekana kutokuwa na msaada hata kabla ya Banda kulambwa kadi.

 Kiungo cha ukabaji kiliruhusu makosa zaidi ya matatu ndani ya dakika 15 za mwanzo. Lakini hata baada ya kurudishwa nyuma kusaidiana na Juuko Murshid, hakuwa anaweza kuruka kupiga mipira ya vichwa na kasi yake ukilinganisha na alivyo Ngoma au alipoingia Simon Msuva, kila akiingia ndani ni tatizo kwa kuwa Majabvi ananyata, huenda ni umri ndiyo unamtupa mkono.

 Hivyo kama angetolewa yeye, akaingizwa Lufunga, Mwinyi Kazimoto angecheza namba nane na namba sita angekaa Mkude. Pamoja na Said Ndemla, watatu hao wangetengeneza ‘triangle’ ambayo bado ingeweza kuivuruga Yanga na kuipa Simba uhai.

Najua, kulikuwa na ugumu kwa kuwa pungufu halafu ukatangulia kufungwa. Lakini kasi dhaifu ya Majabvi, ufupi wake pia. Ukilinganisha na kasi ya fowadi ya Yanga, pia lilikuwa ni tatizo.


Yanga ingetulia, ingeweza kupata mabao zaidi na kuiadhibu Simba zaidi. Hata hivyo, mechi imepita na Simba wanapaswa kujifunza kupitia makosa na si kutengeneza majipu ambayo yanaweza yakasababisha wao wenyewe kutumbuliwa na kuvurugikiwa kabisa.

2 COMMENTS:

  1. Saleh acha unazi wewe,Simba kafungwa kwavile hakujiandaa kucheza na wazoefu zaidi ya timu kama JKT,Majimaji nk

    ReplyDelete
  2. naona umezungumzia mapenzi lakini ukweli umeusema wazi kwamba alimtangulizia mguu kisha akamsukuma na bega!! Huko ni kumtega na sheria ziko wazi huwezi kumchezea faulo mbili mchezaji halafu lefa akakuacha!! Inajulikana unapomfanyia faulo ukiwa ni mtu wa mwisho njano amekuhurumia ila huwa ni straight red card!! Yule dogo alikuwa na mentality moja ya kumtoa Ngoma mchezoni ila akasahau kuwa tayari Yanga waliishalijua hilo na wakamuandaa kisaikolojia na jinsi ya kutumia udhaifu huo

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic