Na Saleh Ally
MIAKA minne au mitano iliyopita, kulikuwa na watoto wanaokwenda Ujerumani kwa ziara ya kimichezo. Hawa walikuwa ni wale wa kituo cha TSC cha Mwanza.
Baadhi walijumuishwa wachezaji wachache kutoka nje ya Jiji la Mwanza lakini wachache wakaenguliwa katika safari hiyo akiwemo Hassan Isihaka.
Waliopata nafasi ya kwenda walikuwa ni pamoja na Said Ndemla aliye Simba sasa, Miraji Madenge ‘Sheva’, Japhet Vedastus, Carlos Protus hawa wako Toto Africans, Frank Sekule, alikuwa Simba sasa yuko Majimaji na wengine.
Isihaka alikosa nafasi ya kwenda Ujerumani kwa kuwa mmoja wa wahusika raia wa Ujerumani ambaye ni rafiki yangu alionyesha wazi kutoridhishwa na uwezo wa wake, tena akasisitiza alikuwa akitumia mguu mmoja tu, jambo ambalo si sahihi kwa beki wa kati.
Miaka michache mbele, Isihaka akaanza kung’ara na timu ya vijana ya Simba ambao walikubali kuendelea kumlea hadi alipopanda katika kikosi cha kwanza.
Kama unakumbuka Oktoba 18, 2014, Simba iliwashangaza watu wengi baada ya kuwatumia vijana wawili katika mechi kubwa dhidi ya watani wake Yanga. Vijana hao walikuwa Peter Manyika na Isihaka. Mechi ikaisha kwa sare ya bila bao, kuanzia hapo, vijana hao wakaanza kuaminika.
Miezi michache baadaye, mitandaoni akaonekana Isihaka akiwa kwenye picha karibu na kiongozi wa Simba akisaini mkataba wake mpya na taarifa zikasema, atakuwa na mshahara mnono.
Msimu huu, hata kabla haujaisha, Isihaka amefungiwa kutokana na kumuonyesha dharau Kocha Mkuu, Jackson Mayanja, eti kwa kuwa hakumpanga katika mechi dhidi ya Yanga.
Taarifa zinaeleza, Mayanja alitaka kumpanga Isihaka aitumikie Simba katika mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Singida United. Naye akamhoji kama likizo yake ya kukaa benchi imeisha. Maana yake Mayanja ndiye alitakiwa kujieleza kwa Isihaka.
Uongozi wa Simba ukaamua kumsimamisha kwa muda usiojulikana. Hapa ndipo yanapoanzia masikitiko yangu ambayo nayaunganisha na kumbukumbu, pia nitajumlisha na pole.
Jana, Isihaka alijitokeza na kuomba radhi akiwa ametambua alichokifanya ni tatizo kubwa. Hilo ni jambo la kiungwana kabisa na vizuri ikawa ameomba msamaha kutoka moyoni na aone amelijutia suala hilo. Lakini si ameomba radhi kwa kuhofia kuondoa Simba huku alichofanya akiona si sahihi.
Kwa suala la kuomba radhi ninampongeza, lakini kwa kuwa nilitaka kumueleza, basi acha niendelee.
Zaidi ya mara moja, nimeeleza kuhusiana na kuliona kosa la Simba kumpa unahodha, mwanasoka kinda kabisa huku akiwa anaongoza wakongwe wengi. Nilieleza namna ambavyo walikuwa na haraka na hakustahili “kitambaa” hicho cha klabu kama Simba.
Nilieleza namna Isihaka ambavyo amekuwa akizungumza na vyombo vya habari, hakika hakuonyesha sifa za kuwa nahodha. Tena alionekana hakustahili hata kuwa nahodha wa timu ndogo ya ligi kuu, nikasema anahitaji muda.
Lililotokea kwa Mayanja, linaonyesha hakika bado hajajitambua, ni mambo ya kitoto kabisa. Heshima kwa kiongozi ni jambo jema. Kutopangwa mechi ya Yanga, hakuwezi kuwa mwisho wa kuitumikia klabu yako, kwani Isihaka hajaona nyota kibao hawajacheza mechi dhidi ya Yanga?
Maana ilikuwa ni vita ya viongozi mbele ya watumishi wengine wa Simba. Kocha na nahodha ni viongozi, lolote walipaswa kulizungumza pembeni. Kama Isihaka hakufurahia kuwekwa benchi, basi angemuona kocha pembeni kuliko kumjibu ‘shombo’ mbele ya wachezaji wengine, tena bila ya nidhamu.
Lakini hebu jiulize, hivi Isihaka asipopangwa kwenye mechi dhidi ya Yanga ni sahihi amdharau kocha. Wewe unaweza kunikumbusha kutokana na kipi hasa? Mussa Hassan Mgosi yuko benchi, mkongwe na mzoefu kuliko Isihaka mara mia, mwenyeji Simba kuliko Mayanja, kaifunga Yanga kuliko Kiiza, Ajib na bado yuko kimya. Isihaka ni nani kabisa?
Simba walimuwahisha. Kijana anajitahidi lakini mambo mengi bora au mazuri yanahitaji muda. Isihaka ana mengi sana ya kujifunza, apewe nafasi lakini naye anapaswa kujitambua. Anaweza kuondoka Simba leo ikawa ndiyo ‘safari’ kabisa.
Wako wengi wana vipaji, lakini wamefeli kutokana na ukosefu wa nidhamu. Mniamini, nidhamu mbovu, imewafelisha wengi hata wenye vipaji, pia fedha.
Kingine niwakumbushe wadau, siamini kama ni sahihi eti kuulaumu uongozi wa Simba kumchukulia hatua mchezaji anayemdharau kocha tena mbele ya wachezaji wengine.
Masikitiko ni kwamba viongozi Simba wameamua kumwamini haraka lakini mhusika hakulitambua hilo na sasa anataka kumpanda kila mtu kichwani. Lazima tuwaunge mkono wanaopambana kuwafanya vijana wawe bora. Kwa kuwa Isihaka ameomba radhi kwa kocha wake basi, naye amsamehe, amfunze zaidi na Simba wasihangaike kukata mkono kwa sababu mtoto akinyea mkono…








0 COMMENTS:
Post a Comment