March 2, 2016

KIKOSI CHA SIMBA KILICHOING'OA ZAMALEK

Na Saleh Ally
Katika historia ya Tanzania, moja ya miaka itaendelea kubaki kwenye kumbukumbu ya mafanikio kwa miaka mingi ni 2003.

Hii ni wakati Simba ilipofanikiwa kuivuruga kabisa Zamalek ya Misri na kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Nakumbuka wakati Simba inarejea nyumbani ndiyo yalikuwa mapokezi makubwa zaidi ya timu kupokelewa na mashabiki na wadau wa soka kuliko yoyote yale yaliyowahi kutokea.

Baadhi ya watu walipoteza maisha, Mwenyezi Mungu awarehemu huko walipo.
Historia na rekodi, mara nyingi ni bora pale mnapozungumzia suala la rekodi. Vizuri kujifunza na mengi.

Baada ya Simba kuivua Zamalek ubingwa wa Afrika, wakati huo ikiwa ndiyo timu bora ya Afrika, tena ikifanyiwa hivyo kwao. Hakuna timu nyingine ya Tanzania imewahi kuonyesha jeuri hiyo ikiwemo Simba yenyewe.

Haikuwa hazi ndogo, kuifunga Zamalek bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru).

Halafu Simba ikasafiri hadi Oman, huko ikaweka kambi. Kocha Mkuu, James Aggrey Siang’a akashirikiana na Talib Hilal kuiweka Simba sawa.

Ikatua Cairo. Dakika 90 zikaisha Simba ikiwa imelala bao 1-0. Hata dakika zilipoongezwa, matokeo yakabaki hivyohivyo na mikwaju ya penalti Kaseja akabuka shujaa wa kupangua na Christopher Alex akamalizia kazi ya kuwang’oa matajiri hao wa Kiarabu.

Sasa linakuja swali ambalo ninataka tutajadili. Ukiangalia kikosi hicho kilichofanya maajabu Cairo, yaani wale wachezaji 11 walioanza, mgeni alikuwa mmoja tu.

Beki wa kushoto, Ramadhani Wasso. Kumi waliobaki ni wazalendo, Watanzania kutoka katika mikoa mbalimbali kama Kigoma, Kagera, Kilimanjaro na kwingineko.

Kipindi hiki wakati klabu za Yanga, Azam FC na hata Simba, pia nyingine zikiendelea kutumia fedha nyingi kusajili wageni lakini zinashindwa kabisa kufikia hatua kama hiyo.

Hatua ambayo ilifikiwa na Simba miaka 13 iliyopita ikiwa imejaza wachezaji wazalendo kibao ambao walifanya kazi yao vizuri.

Tunaweza kujifunza kwa wazalendo hao, kwamba ilikuwaje hadi wakaing’oa Zamalek iliyokuwa katika kiwango bora na si kama Zamalek ya sasa?

Wageni vipi wameshindwa kuwa chachu ya kusaidia kufikia mafanikio zaidi wakiwa wanalipwa mamilioni kibao kuliko wazawa?

Tujiulize, kweli viongozi wa klabu wanawauwa wachezaji wazawa kwa kutumia nguvu nyingi kuwalipa wachezaji wa kigeni?

Vipi waliweza kina Kaseja wanashindwa akina Barthez. Inakuwaje Pawasa na Costa walifanikiwa na Cannavaro na Yondani hawawezi?

Gabriel au Batigol, Uli Mwakingwe na wenzao walifanya vema. Lakini Paul Nonga, Simon Msuva na wengine hawawezi leo! Tatizo lipo na kikosi hicho cha Simba kinazungumza.

Ukiwaona wachezaji hao walivyokaa inaonyesha pamoja na wachezaji wageni kuwa chachu, bado kuna jambo linatakiwa kufanyika kwa wachezaji wazawa.

Kizazi cha sasa, ndiyo kizazi cha kina Kaseja, Matola, Pawasa na wengine. Vipi wale waliweza na hawa wanashindwa?
Lakini pia ni somo kwa wachezaji wenyewe wajue kabisa kama wanastahili kujituma, kujiamini na hawapaswi kufa moyo. Wanaweza kukitumia kikosi hicho cha wazawa cha Simba kama sehemu ya mfano ya maisha yao ya soka.

KIKOSI CHA SIMBA KILICHOING'OA ZAMALEK
1. Juma Kaseja
2. Said Sued ‘Panucci’
3. Ramadhani Wasso
4. Boniface Pawasa
5. Victor Costa
6. Selemani Matola
7. Ulimboka Mwakingwe
8. Christopher Alex
9. Emmanuel Gabriel
10. Yusuf Macho ‘Musso’
11. Athumani Machuppa

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic